Wanaotaka kuvunjwa kwa SUK Zanzibar, wachukue tahadhari kabla ya hatari

Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano (katikati) Mzee Hassan Nassor Moyo akiwa na Maalim Seif Sharif Hamad na Dk Amani Abeid Karume ambao walifikia Maridhiano Novemba 9, 2007 na kuviweka Visiwa vya Zanzibar katika hali ya amani na utulivu
Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano (katikati) Mzee Hassan Nassor Moyo akiwa na Maalim Seif Sharif Hamad na Dk Amani Abeid Karume ambao walifikia Maridhiano Novemba 9, 2007 na kuviweka Visiwa vya Zanzibar katika hali ya amani na utulivu.

Salma Said,

Zanzibar. Licha ya kuwepo kwa maelewano yaliyotokana na kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa kumekuwa na mawazo tofauti kwa baadhi ya wanasiasa Visiwani Zanzibar wakitaka kurejea hali ya mwanzo na kuachana na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyovishirikisha vyama viwili vikuu visiwani humo vya CCM na CUF.

Baadhi ya wanasiasa wanaukosoa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa hauna tija kwa siasa za Zanzibar, wengine wakiuelezea mfumo huo kuwa umeiweka Zanzibar katika siasa za kileo za ushindani wa hoja.

Miongoni mwao wanataka Umoja huo ukome na kurejea hali iliyokuwa mwanzo ya siasa za ushindani wa nguvu na zisizo na maelewano.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama cha Mapinduzi na Mwakilishi wa viti maalum CCM, Asha Bakar Makame, mara kadhaa ametamka hadharani nia yake na ya baadhi ya wawakilishi wenzake kutaka kuwasilisha hoja binafsi ili kuondokana na mfumo huo.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin, nae anaipinga wazi wazi SUK na kutamka hadharani dhamira yao ya kuwasilisha hoja binafsi kutaka Zanzibar irejee katika mfumo wa anayeshinda kuchukuwa kila kitu.

Wiki iliopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na mabalozi wa nyumba kumi wa chama chake, pamoja na mambo mengine aliwaeleza ikiwa hawautaki mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni lazima CCM ishinde kwa kura nyingi zaidi, lakini pia suala la mfumo huo limo ndani ya Katiba Zanzibar.

Historia ya siasa za Zanzibar

Historia ya siasa Zanzibar inaonesha kuwa tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza mwaka 1957 hadi mwaka 2010 hakuna Chama cha siasa kilichoweza kupata kura nyingi zaidi na kwamba matokeo ya chaguzi hizo ni kura kukaribiana.

Ni muhimu kuelewa kuwa kuwepo kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hakukuja ghafla bali kumefuatiwa na makubaliano yaliofikiwa na viongozi wawili wakuu vya vyama vya kisiasa, Amani Abeid Karume (CCM) na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad.

Novemba 5, 2009 wazanzibari wengi walishangaa kusikia Maalim Seif amekwenda Ikulu Mjini Zanzibar na kupeana mkono na Amani Karume, wakati ambapo siasa za chuki zikipamba moto na hakuna aliyetarajia tukio hilo.

Viongozi hao wawili, walikubaliana mambo matatu ya msingi ambayo waliamini yangeweza kuivusha Zanzibar pale ilipo na kwenda hatua nyengine mbele za kisiasa, kimaendeleo, kiuchumi, kujenga misingi ya udugu, upendo na kuendesha siasa za ushindani wa hoja.

Makubaliano hayo yaliitwa jina la Maridhiano, yaliotokana maneno ya Tusameheane, Tusahau yaliopita na Tusonge mbele. Hiyo ndio siri ya mafanikio ya maridhiano yalikuwa yakisakwa kwa miaka kadhaa Zanzibar.

Maoni ya wadau

Wadau wa amani, utulivu na siasa za maelewano wanatoa angalizo kwa wanasiasa visiwani Zanzibar kuacha mara moja mpango huo waliouita hatari kwa maelezo kuwa utavirejesha visiwa hivyo katika hatari kubwa kuliko iliyokuwa mwanzo.

Wanawakumbusha wanasiasa na wananchi kwa ujumla wao, kurejea nyuma hali ilivyokuwa katika visiwa hivyo kabla ya kuundwa kwa SUK na kuangalia hali iliyopo sasa na kutathmini ni ipi njia njema inayofaa kufuatwa.

Padri wa Kanisa la Anglikan Zanzibar, Emmanuel Masoud anasema kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kumeleta mafanikio makubwa katika kudumisha hali ya amani na utulivu na pia kutoa fursa ya wananchi wa visiwa hivyo kuendelea kwa shughuli za kijamii bila usumbufu kama ilivyokuwa awali.

 “Mimi ni muumini wa Maridhiano na naipigia debe sana kwa sababu dini inatutaka tuishi pamoja kwa maelewano na udugu na hali hiyo ndio walioturithisha wazee wetu walikuwa wakiishi kwa pamoja ” amesema Padri Masoud.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) Sheikh Muhiddin Zubeir Muhiddin anasema serikali ya umoja wa kitaifa imeleta maelewano amani na utulivu mkubwa na kuondosha mgawanyiko katika kipindi cha miaka minne huku akishauri kuendelezwa kwa Maridhiano na mfumo wa serikali ya umoja.

 Naye Jack Jacob Mwakingila Mwalimu wa Jumuiya ya Inter Faith anasema “Ninachokiona kwa upande wa utulivu wa nchi upo kidogo ila siku za hivi karibuni baada ya kumalizika kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba kumejitokeza hali ya kutoleana maneno yasiofaa, matusi na kejeli ambazo hazileti afya katika nchi yetu” anasema.  

Mwakingila anasema kwa upande wa ukuaji wa uchumi wa nchi bado mwananchi hajaona manufaa yoyote kwa kipindi hiki cha miaka minne kwa kuwa hali za maisha ni mbaya na maisha ni magumu sana kwa watu wa hali ya chini  na akaishauri serikali kufanya juhudi za makusudi kurekebisha hali hiyo.

Mohammed Yussuf aliwahi kugombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, anasema SUK imesaidia sana katika kuleta na kuboresha hali ya amani na utulivu.

Anasema ni SUK ndio iliyojenga utamaduni mzuri wa majadiliano na mashirikiano miongoni mwa wananchi bila ya itikadi zao za kisiasa.

 “SUK imefanikiwa sana hasa katika kipindi cha miaka mitatu ya awali tokea kuanzishwa kwake, kujenga imani na upendo baina ya viongozi na wafuasi wa CCM na CUF. Hata hivyo, GNU ina changamoto zake ilipaswa kutekelezwa katika ngazi za mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi wakuu wa mikoa na wilaya hadi masheha” alisema.

Anasema kukosekana kwa msimamo wa pamoja kuhusu mchakato wa Katiba kuna athari mbaya ya kuhatarisha uhai wake, tayari kauli za chuki na uhasama zimeanza kujitokeza ambapo viongozi wa pande zote mbili lazima waachane na kauli hatarishi ikiwa wanataka Serikali ya Umoja wa Kitaifa iweze kudumu.

Mkurugenzi wa CUF, Salim Bimani anasema hakuna anayeweza kubeza mafanikio ya Maridhiano isipokuwa wale ambao hawataki kuiona Zanzibar ikiwa na amani na utulivu.

 “Hao wanaosema wamechoshwa na serikali ya umoja wa kitaifa hawasemi ukweli lakini tusipate tabu maana hawa hawa ndio madalali wa kuiuza Zanzibar na ndio wale wale walioipinga wakati wa kura ya maoni” anasema Bimani.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti la Mwananchi, wanasema pamoja na kasoro zilizopo katika SUK, bado wanaona faida ni nyingi zilizopatikana chini ya mfumo huo na hapa wanakumbusha hali ya misukosuko ya kisiasa ya wakati huo.

Masoud Faki Masoud anasema wananchi wa kawaida wameona faida ya miaka minne ya serikali ya umoja wa kitaifa kwani siku za nyuma kulikuwa na ubaguzi na uhasama ambao ulitokana na tofauti za kisiasa.

Ni mwaka mmoja umebaki kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu hapo mwakani, lugha za kimaridhiano zimeanza kutoweka ustaarabu umeanza kupungua vitisho na ubabe unaanza upya, Je, tumechoshwa na Maridhiano?

Suleiman Khalfan Ali, mkazi wa Kibuteni Wilaya ya Kusini Unguja, anasema hali tete ya kisiasa Zanzibar ni ya muda mrefu, tokea kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa Tanzania mwaka 1992.

 “Tumeshuhudia kuharibiwa kwa chaguzi, mbegu za ubaguzi, chuki na hasama za kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa 1995 ambao ulimuweka madakarani Dk Salmin Amour Juma, chuki na hasama za kisiasa zilifikia hadi kutouziana bidhaa madukani na kutozikana jambo lililochangia kurejesha nyuma maendeleo, hakuna mwananchi anayependa kurejea kwa hali ile” Anasema Suleiman.

Makame Hamad Faki, mkazi wa Mchangamdogo Wilaya ya Wete, anasimulia madhila ya siasa za chuki na hasama kwa wakati huo;“Sisi ni mashuhuda wa siasa hizo za chuki na hasama, ni waathirika wa chaguzi hizo wapo waliopigwa na kubaki vilema…kusema tuvunje au tuachane na umoja wa Kitaifa ni kutaka kurejesha madhila kwa wananchi visiwani hapa” anaongeza.

Historia na matokeo ya siasa za uhasama

Mwaka 2001 watu kadhaa walipoteza maisha yao na kwa mara ya kwanza Tanzania iliingia katika historia ya kutoa wakimbizi waliokimbilia nchi jirani za Kenya eneo la Mombasa na Somalia.

Kufuatia hali hiyo, viongozi wa Afrika walianzisha jitihada za kutafutwa kwa ufumbuzi wa kisiasa ambapo Juni 9, 1999 Mwafaka kwanza uliosimamiwa na Jumuiya ya Madola chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake kwa wakati huo, Chifu Ameka Anyauku ambapo Maalim Seif na Haji Mkema walitia saini Muafaka huo ambao haukuweza kutekelezwa.

Hali ya kisiasa Zanzibar ilimsononesha kila mpenda demokrasia. Juhudi za kutafuta suluhu ziliendelea na ilipofika Oktoba 10 mwaka 2001 vyama vya CCM na CUF vilifikia muafaka na kutia sahihi makubaliano katika Ikulu ya Zanzibar huku Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa akiwa shuhuda.

Kwa kiasi fulani kulikuwa na utekelezaji wa Muafaka wa pili, ingawa yapo mambo kadhaa ambayo hayakutekelezwa, lakini Serikali kwa upande wake iliweza kuwasilisha marekebisho ya Katiba ya Zanzibar, yalifanyika marekebisho ya nane na ya tisa yaliyoweka mambo sawa hasa Tume ya Uchaguzi na sheria za uchaguzi, kuanzishwa kwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka na masuala mengine.

Rais Kikwete naye alijaribu kutaka kutafuta ufumbuzi na vikao vya pande mbili vilikaa miezi 18 lakini ilishindikana. Lakini Amani Karume na Maalim Seif walipoamua waliweza kukaa pamoja na kutaka kumaliza uhasama wa vyama vyao vyenye nguvu sawa katika visiwa vua Unguja na Pemba.

Baraza la Wawakilishi, Januari mwaka 2010 lilijadili hoja ya mapendekezo ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa iliyowasilishwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mgogoni (CUF), Abubakar Khamis Bakar.

Siku chache Mswaada wa Sheria ya kura ya maoni ukawasilishwa ndani ya kikao cha Baraza la Wawakilishi na ukaungwa mkono na pande zote mbili za wajumbe kutoka CCM na CUF na hatimae kura ya maoni ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikaratibu zoezi la uchaguzi wa kura ya maoni na hatimae Wananchi wakapiga kura ambapo asilimia 66.40 ya wazanzibari wakaunga mkono muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa huku asilimia 33.90 ikipingana na mfumo huo.

Dondoo:

Matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyompa ushindi rais wa sasa Dk Ali Mohamed Shein yalitangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Khatib Mwinchande ambaye alimtaja Dk Shein kushinda uchaguzi huo kwa asilimia 50.1 huku Maalim Seif akipata asilimia 49.1 hali iliyopelekea kiongozi huyo wa CUF kuwemo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa visiwa hivyo akitokea chama pinzani.

 Chanzo: Mwananchi

 

 

Advertisements

One Reply to “Wanaotaka kuvunjwa kwa SUK Zanzibar, wachukue tahadhari kabla ya hatari”

  1. Tatizo la Maridhiano ni kwamba walioridhiana ni Amani na Seif Sharif kwa niama ya vyama vyao bila ya ridhaa za dhati za wanachama wao .Pili ,ni kwamba mfumo wa SUK umejisheheni sana kuhusu mgawano wa vyeo tokea umakamo wa Urais na Mawaziri – lakini Ilani na sera utekelezaji ni za CCM .Tatu ,ni kwamba Maridhiano yasiyo na lengo la kubadili “mindsets za wananchi ” wa kawaida,na kuwepo nidhamu ya kuheshimiana kuhusu misimamo ya kisiasa bila ya kejeli na matusi yenye misingi ya siasa za 1957 – 1963 Maridhiano hayo yatakosa radhi za jamii .Nne ni lazima ieleweke kamba vyama vikuu 2 Visiwani vinatofautiana Kiitikadi hasa katika suala la siku ya Uhuru wa kweli wa Zanzibar ,suala la kuuondoshwa Ufalme ,suala la Mapinduzi na bila ya shaka hii suala sugu la aina mfumo wa Muungano na khasa Rasimu Pendekezwa .Maridhiano ya yaliyo na msingi wa “amri za wakuu ” bila ya Ridha safi za wananchi ni kuleya unafiki wa kisiasa wa ama “uchu wa madaraka au kun`gan`gania utawala kwa hasara ya maendeleo nchini

    Matamko makubwa-makubwa ya viongozi kwamba “.tusameheane na tusahau yaliyopita pasina usahihi wa nia safi hautaeleta salama na amani visiwani katika chaguzi zijazo,kwa sababu wapo
    walikwisha anza za kusambaza sumu za eti za kuvaa mabuti na kwamba ikiwa hawatapewa ushindi hapatokalika .Hii ndio hatari ambayo inatumiliwa sana wachache ambao ni wapotoshi wenye kupenda Ukubwa wasiostahiki kwa hali yeyeote – ya kuendesha nchi .Hawa ndio wale wenye kelele-kelele nyingi mitaani .

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s