Uwanja wa siasa Z’bar rafu

dksheinmaalimseifNa Jabir Idrissa

UWANJA wa siasa Zanzibar unachafuka kadri siku zinavyoenda kuelekea uchaguzi mkuu 2015. Wakati viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakivutana na kufitiniana, uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein umetunisha misuli dhidi ya raia.

Gazeti hili limefuatilia hali ya mambo ya kisiasa Zanzibar, ikiwemo ndani ya CCM, na kubaini Dk. Shein ameanza kukabiliana na makada wenye nia ya kumzuia kutetea kiti chake katika uchaguzi wa Oktoba mwakani.

“Hata kauli zake ni za kutishia kuwashughulikia wale anaowaita ‘watu wanaochochea uvunjifu wa amani na utulivu’. Hili linazidi kumbomolea imani kwa wananchi,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BW) ambaye hakupenda kutajwa jina.

Dk. Shein amekuwa akishambulia viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao wamekuwa wakieleza jinsi baadhi ya mambo yanavyokwenda serikalini, ikiwemo pale wanapoona rais amekosa kuonesha uongozi madhubuti kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar.

Ndani ya CCM

Akihutubia viongozi wa mashina pamoja na maskani wa Wilaya ya Mjini, juzi Jumatatu, Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, alisema hajamtuma mtu kusema kuwa hatagombea tena.

“Sijawahi kuzungumza na mtu yeyote juu ya suala la kugombea. Sasa kwanini watu wengine wanisemee wakati mimi mwenyewe nipo?” aliuliza wakati wa mkutano wa ndani uliofanyika Hoteli ya Bwawani.

Dk. Shein amesema wapo watu “wanapita huku na kule kueleza kuwa mimi sitagombea nafasi ya urais katika uchaguzi ujao; mbona mimi mwenyewe sijawahi kutamka?”

Amesema yeye hakurukia siasa, kwani aliingia tangu akiwa darasa la nne wakati wa Afro-Shirazi Party (ASP), kiasi cha kuwahi kufukuzwa shule; na kwamba anaheshimu chama chake na utaratibu wa kupata wagombea, lakini wakati wake haujafika.

“Msivamie mambo; hayo mnayopita mkisema hayawasadii kitu. Kama hamyajui, mimi mwenyewe nipo niulizeni, lakini siyo kusema yasiyostahiki,” amesema.

Hakutaja yeyote katika viongozi waandamizi wa CCM, lakini gazeti hili limefahamishwa na vyanzo ndani ya chama hicho kuwa wapo viongozi wawili – mmoja kutoka serikali ya Rais Jakaya Kikwete na mwingine katika serikali anayoiongoza Zanzibar – walio katika mikakati ya kuusaka urais.

Taarifa zilizoenea mitaani Zanzibar zinasema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilali, ndio wanajipanga kwa urais Zanzibar.

Dk. Shein amesema ni muhimu kwa viongozi kuheshimiana na kwamba yeye amekuwa akimheshimu kila mtu, mkubwa kwa mdogo, na kuongeza kuwa kama wako walio na hoja dhidi yake, basi wasubiri wakati wa uchaguzi utakapofika.

Dk. Shein ambaye alitangazwa mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba 2010, anatarajiwa kukamilisha ngwe yake Oktoba mwakani.

Wachunguzi wa siasa za Zanzibar wanasema, uongozi wake wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa unaonekana “kujaa visirani;” upande mmoja vikichangiwa na staili yake ya kutozingatia mahitaji halisi ya wananchi tena bila kuwabagua; na kutokuwa na msimamo madhubuti kwa mambo yanayoonekana ni muhimu kitaifa.

Dk. Shein amepata wakati mgumu hasa pale kunapokuja suala linalohusu ushirikiano na serikali ya Rais Kikwete kwa kuwa, hata kama linakuwa jambo la kujali zaidi maslahi ya Zanzibar, anaamini zaidi kukitetea na kukilinda chama atokacho.

Hili linachukuliwa kuwa ni “kuzorotesha ushirikiano wake na mshirika wake mkuu katika serikali,” Maalim Seif wa CUF; na hivyo kuchukiza Wazanzibari wanaochagua upinzani.

Mfano mzuri ni suala la upatikanaji katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ambapo alishindwa kusimamia serikali kupata sauti moja na kuikomaza kwa wajumbe wa Bunge Maalum wa CCM na upinzani watokao Zanzibar; na hivyo kuacha washiriki vikao Dodoma kubaki wamegawanyika.

Wakati anakabiliana na wale wanaojiamini kuwa wanaweza kumrithi mapema, Dk. Shein analazimika kukabiliana na mgawanyiko uliopo katika chama.

Vyanzo vya taarifa vinasema kazi kubwa inayomkabili sasa ni kusimamia mkakati wa kushawishi kuikubali Katiba Inayopendekezwa ambayo ilipitishwa na Bunge Maalum la Katiba, lililokuwa na asilimia 80 ya wana-CCM.

Katiba hiyo haikubaliki kwa washirika wake katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), wakiongozwa na Maalim Seif Shariff Hamad.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, ameshasema anaipinga katiba hiyo na ataongoza kampeni ya kuwaambia Wazanzibari waikatae.

Tayari amehutubia mikutano kadhaa Unguja na Pemba na kusema katiba hiyo “haiifai Zanzibar” kwa kuwa inaizamisha kwa kuipora mamlaka inayoyahitaji ili kujiendesha kiuchumi.

CUF imeungana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kupinga katiba hiyo.

UKAWA uliundwa wakati Bunge Maalum lilipoanza mjini Dodoma, na pale wenyeviti wa vyama hivyo walipojiridhisha kuwa CCM ilipanga mkakati wa kuvuruga Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba, ili kushinikiza rasimu inayokidhi maslahi yake.

CCM imo katika harakati za kuhakikisha katiba hiyo inapita katika Kura ya Maoni iliyopangwa kufanyika Aprili mwakani. Wakati inaamini si kazi kubwa kupata ushindi Tanzania Bara, kibarua kiko Zanzibar.

Kiongozi mwandamizi wa CCM ambaye amepata kuwa waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mjumbe wa Kamati Kuu, amebainisha hali hiyo ngumu katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.

Anasema mikutano iliyokusudiwa kushawishi wananchi waipigie kura ya NDIO katiba inayopendekezwa, inatumika kwa viongozi kujijenga kisiasa majimboni mwao.

Anasema mikutano hiyo inatawaliwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, huku ikiwatenga wabunge, hali ambayo anasema inadhalilisha wabunge mbele ya wananchi kwa kuonekana hawawatumikii vema wananchi.

Kada huyo anakiri kwamba wabunge wengi na wawakilishi hawaelewani. “Jambo hili linazidisha msuguano katika wakati ambapo mshikamano unahitajika sana,” anasema katika mazungumzo yake na Kinana.

Lakini kiongozi huyo anashauri anachoona ni kwa maslahi ya chama chake: “Wasitishe mikutano hii.” Badala yake, anashauri upangwe utaratibu mpya kwa ushirikiano wa Kamati za Siasa za Majimbo na Wilaya; ajenda zikiwa ni katiba inayopendekezwa.

Kwa mujibu wa kada huyo, mikutano inayofanyika majimboni inaratibiwa na Balozi Seif na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.

Anasema kwa sasa, mikutano hiyo imesitishwa kwa sababu Balozi Seif yuko ziarani nchini China; bali anasema “akirudi ratiba itaendelea.”

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s