Wanashughulishwa na bendera? Ni kwisha kisiasa

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai

SIMO katika wananchi wanaolaumu ubaya wa serikali ya umoja wa kitaifa (SUK). Hapana. Mimi nishatoka hapo, ninavoisema serikali, wewe msomaji ujuwe ninamlaumu Dk. Ali Mohamed Shein kama kiongozi mkuu Zanzibar.

Kwa hivyo, mwanzo kabisa wa mjadala huu leo, nifahamike namtupia lawama Daktari kwa sababu ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyeapa kutumikia Zanzibar.

Na kwa sababu ninamlaumu Dk. Shein kwa sababu ndiye kiongozi mwenye dhamana kuu ya umma kuiongoza Zanzibar, yenye mchanganyiko wa wananchi, na mchanganyiko wa fikra na misimamo vilevile, basi nawatoa lawamani na shutumani viongozi waliomo Baraza la Mawaziri, wanaotoka Civic United Front (CUF) Chama cha Wananchi.

Viongozi wa CUF walioko ndani ya safu ya mawaziri wa Rais Dk. Shein, nataasaf kwamba hawahusiki na ujinga mkubwa wa kiuongozi unaofanywa na serikali anayoiongoza Daktari.

Ni kweli Dk. Shein anaongoza SUK. Lakini kwa mambo yanayofanywa na serikali, si rahisi kuwajumuisha mawaziri aliowateua kutokea CUF. Viongozi hawa hawahusiki kwa kweli na uovu unaodhoofisha umoja wa kitaifa Zanzibar.

Hicho sicho walichoahidi kukitekeleza kwa umma. Waliahidi neema chini ya misingi ya uongozi ulio mwema. CUF haijapata kuahidi ujinga. Haijaahidi watu ukandamizaji. Ni CCM wanaostawisha ukandamizaji.

Hili si jambo la ajabu na uongo. Hili lipo kwenye rekodi wazi. Serikali zao zote mbili, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na SMZ, zinaua raia, achilia mbali kuwanyima haki zao za msingi. Kuwatesa na kuwadhalilisha.

Kwa sababu hiyo basi, nataka ieleweke vizuri, Dk. Shein anaingia lawamani kwa sababu kwa muda mwingi anakaa zaidi na mawaziri wanaotokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

CCM ndio chama atokacho yeye. Ni chama hichi kilichomteua Dk. Shein agombee urais mwaka 2010. Ni viongozi wa chama hichi waliopanga kwa namna mbalimbali na wapuuzi katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar – Zanzibar Electoral Commission (ZEC) – kupika matokeo ya urais na hatimaye Dk. Shein akatangazwa mshindi.

Jambo hili lilikuwa likiwahangaisha Wazanzibari wengi kwamba ni kweli ndivo ilivyokuwa pale wakati umma wa wananchi wakisubiri matokeo yatangazwe kupitia hadhara iliyokutanishwa ndani ya ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani?

Mwenyeezi Mungu ameleta kudra yake na kuwatoa hofu wananchi juu ya utata wa matokeo yale yaliyotangazwa na Tume. Amelisema hili kwa uwazi muasisi wa Mapinduzi, Muungano na CCM, mzee Hassan Nassor Moyo – Dk. Shein “alitangazwa tu rais.”

Mzee Moyo, memba wa CCM anayeshika Kadi Na.07 ya uanachama, anasema yeye ndiye aliyeongoza ujumbe   wa kwenda kumshawishi Maalim Seif Shariff Hamad akubali matokeo ya kushindwa. Maana yake aliyetangazwa mshindi, hakushinda kweli.

Watu wanakumbuka hali iliyotangulia utangazaji wa matokeo yale yaliyompa ushindi Dk. Shein.

Wanakumbuka umma ulivoshtadi kwenye geti la kuingilia Bwawani. Pale viongozi wakubwa walipopeleka salamu kwa viongozi wa CUF, eti wakawatulize na kuwapa matumaini kuwa hakuna lililoharibika.

Hali ilikuwa mbaya. Ilikuwa mbaya kwa sababu wapigakura waliokusanyika Bwawani, asilimia kubwa walikuwa ni wafuasi wa CUF na wapenda mabadiliko. Walitumaini mgombea wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, atakuwa rais wao.

Walikuwa wanayo sababu ya kutumaini hivo. Walizipiga kura nyingi kumuelekea yeye. Waliamini, na bado wanaamini, kwamba yeye ndiye rais wao. Wanamuamini Maalim Seif kuwa ndiye mwanasiasa anayewafaa kuiongoza Zanzibar.

Ukweli huu unajulikana zamani. Maalim mwenyewe alichangia kuchukuliwa mwanasiasa anayeaminika. Alijichunga kiuongozi akijipambanua na viongozi asi kwa wananchi. Alijiweka kiongozi kioo cha jamii katika dhana ya uongozi mwema na mpenda nchi kweli kweli.

Ni mtizamo huo aliouchukua, na kuukomaza kwa wananchi alipotoa ahadi kwamba atakuwa pamoja na Wazanzibari, tena wote wa asili ya Unguja na wote wa asili ya Pemba, akiwa ndani au nje ya serikali. Maalim Seif amekuwa akienenda na ahadi hii aliyoitoa tangu miaka ya 1980 pale utawala ulipoanza kumfanyia visa asiinuke kiuongozi.

Sasa kwa kuwa wananchi wamempa imani Maalim Seif, wanamuamini kuwa ni kiongozi bora anayependa watu, anayezijali raslimali za nchi hii ya visiwa iliyozungukwa na bahari kubwa ya Hindi kwenye pande zote, kila unapokuja wakati wakaipata nafasi ya kupiga kura ya kuchagua   viongozi, wanamtilia yeye.

Kwa hili, wala Wazanzibari hawapapasi kalamu. Wao wakiishika tu karatasi ya kura, kwa sababu dhahiri shahir wanajua kitu wanachokitaka, hawababaiki. Wao taratibu wanatia NDIO penye nafasi ya picha ya Maalim Seif. Wao wanashuhudisha imani yao kwake. Wanamchagua.

Basi Wazanzibari walio wengi walimchagua Maalim Seif hata siku ile ya uchaguzi mkuu tarehe 31 Oktoba, 2010. Kila mtu anajua hamu ya Wazanzibari, ni mabadiliko ya uongozi wa juu wa nchi yao. Akishakaa pale kiongozi wanayempenda, watatumaini mengi ya kheri kuliko kinyume chake.

Wazanzibari wanauhakika Maalim Seif akiongoza nchi, atajitahidi kuondoa shari miongoni mwao. Atajitahidi kushamirisha uongozi mwema, ambao ameuahidi kila wakati wa uchaguzi. Wanaamini atalinda haki zao na kutumia vizuri raslimali zao katika nchi yao.

Wazanzibari wanaamini Maalim Seif ataongoza Zanzibar kwa kuzingatia sheria, imani ya dini yake na mapenzi makubwa kwa watu. Atalinda heshma zao, utu wao, ubinaadamu wao, mali zao, aila zao, matumaini yao.

Katu haiwapitikii akilini mwao kuwa Maalim Seif amekuwa adui wa Wazanzibari leo. Asilan abadan. Wanamuamini angali anakumbuka fadhila za kuaminiwa. Hawezi kuwa kiongozi mpuuzi asiyejitambua. Huyo si Maalim Seif wanayemfaham.

Chini ya uongozi wake Maalim Seif, hakuna mwananchi anayetarajia atakamatwa usiku wa manane nyumbani kwake na kusafirishwa nje ya Zanzibar akatungiwe mashitaka. Hili halitatokea kwa sababu mwenyewe anakemea hadharani ujinga huu.

Akiwa yeye Rais, Maalim Seif hata mara moja hatarajiwi kuagiza serikali yake ikapambane na bendera ambazo ni vitambaa tu walivyochagua wenye asasi yao iliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria za Zanzibar.

Leo Zanzibar ipo kwenye nakama. Inayo serikali inayopambana na bendera za asasi ya UAMSHO – Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam – ambayo ni taasisi iliyopatiwa usajili wa Sheria ya Usajili wa Vyama/Mashirika ya Hiari Zanzibar.

Ni hivi: Msaidizi mkuu wa Rais Dk. Shein anayeitwa Seif Ali Iddi, ambaye kabla ya jina lake hilo anatangulizwa kwa hadhi ya Balozi – utafikiri ni balozi wa maana sana – ametoa amri kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, asimamie askari wa serikali waondoe bendera zote za Uamsho mkoani kwake.

Kwa hivyo, baada ya amri hii, Mkuu wa Mkoa, Juma Kassim Tindwa, amepita akataka wananchi wote wa mkoani anakoongoza, Kaskazini, waziondoe bendera za jumuiya hii ambayo kwa ukweli hasa wanaoifuata ni watu wa dini sana wanaoongozwa na watu wenye upeo mkubwa katika Uislam na asili zake zote.

Wananchi hawakujali amri hiyo. Kwanza, hawaoni kama ni kosa kisheria mtu kuchomeka bendera ya kitu au chama anachokipenda, cha aina yoyote ile hata kama si chama cha siasa. Pili, hawaoni kama bendera tu inaweza kumkosesha mtu usingizi au amani.

Kwamba eti bendera ile nyeupe yenye maandishi tu ambayo si kwamba yanapinga lolote lile la serikali, imnyime raha Rais, au Makamo wake wa Kwanza, Balozi Seif, au mawaziri wa CCM katika serikali ya Dk. Shein, au ikinyime raha chama cha mapinduzi.

Na kama bendera tu ile ya Uamsho inaweza kuwa kero kwa CCM na viongozi wake hao kwa mpangilio huo au hata akiwa ni Katibu Mkuu wao, Abdulrahman Kinana, au Makamo wao wa Bara, Philip Mangula, au hata Mwenyekiti wao, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, basi Watanzania wana shida kubwa na viongozi wao.

Viongozi wanaokasirikia wananchi kwa sababu wamepachika bendera kwenye maeneo yao, lazima waonekane wamefilisika kisiasa. Hao ni viongozi waliochoka kufikiri. Ni viongozi muflis ambao wamejitoa katika kuwa watu wanaowaza ni vipi wataondosha shida tele zinazowakabili wananchi walioapa kuwatumikia.

Ni ujinga mtupu viongozi watu wazima kuacha mambo ya maana katika kuwatumikia wananchi, wakatoa matamko na amri kwa wasaidizi wao washughulike na bendera – vitambaa au matambara.

Hivi matambara ndiyo yanayopambana na umasikini? Hivi matambara ndiyo yanayosaidia serikali kujua kama inapendwa? Hivi matambara ndiyo yanayoizuia serikali kuhudumia wananchi kwa elimu, tiba, maji, na tuseme kufikia malengo ya milenia? Siamini hata kidogo. Bendera haiwezi kuwa jambo la maana sana kwa viongozi wa serikali isipokuwa kama wameishiwa busara kwa kuwa wameshindwa kufikiria njia za kuondoa shida za wananchi.

Viongozi hawa ambao ndio maana nikasema mwanzoni kabisa mwa mjadala huu, kwamba simo katika kuamini kuwa mawaziri waliotoka CUF wanaweza kuwa sehemu ya ushetani huu wa kupambana na bendera. Simo mimi.

Ujinga huu wa kuituma dola ishughulike na bendera ni wa aina yake ambao watu wenye akili nzuri ya maendeleo ya wanadamu hawawezi kushiriki. Viongozi wa CUF waliomo katika SUK pamoja na Maalim Seif hawawezi kushiriki kuagiza upuuzi kama huo.

Dk. Shein yeye anaweza. Kwanini asiweze? Anaweza kwa sababu anayajua yote yanayofanywa na msaidizi wake mkuu, Balozi Seif, wanayetoka pamoja CCM, chama kinachoshika udhibiti wa uongozi wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anajua kwamba serikali yake ndiyo inayohusika kushughulika na bendera, kitambaa, tambara tu jeupe.

Lipo tatizo kubwa Tanzania maana si Zanzibar peke yake. CCM ambayo ndiyo inaongoza dola, imechoka sana. Haina tena nguvu ya kuongoza kama nilivosema hili katika makala mbili zilizopita.

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s