Wa Dk. Shein si ujasiri, ni propaganda chafu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohamed Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Ali Mohamed Shein

CHINI ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein, Zanzibar inasokomezwa. Rais mwenye dhima ya kulea watu na kuijenga nchi kiuchumi, anayoyasema mhh! Serikali anayoongoza inatisha raia, inawavunja moyo. Viongozi hawajali matamshi yao. Wanapayuka. Hakuna kuchunga ulimi.

Kama vile wamesahau lengo la siasa za maridhiano; wanadharau yaliyotumika kufanya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya 2010. Wanachafua amani, utulivu na utengamano.

Hayo matatu ni matunda yaliyokusudiwa kushamirisha utawala bora na utawala wa sheria. Kuleta maendeleo kupitia Serikali ya Umoja wa kitaifa.

Dk. Shein alikula kiapo cha kuongoza vema na kuyalinda maridhiano. Aliahidi kutobagua mtu kwa namna yoyote. Pia aliahidi maendeleo ya watu na nchi.

Yanayofanyika chini ya uongozi wake, na hasa kipindi cha kuelekea mwaka wa uchaguzi mkuu, ni mambo ya ovyo.

Hivi kiongozi hatambui amani na utulivu hutegemea sana uongozi unavyoendesha mambo? Haelewi amebeba dhamana kwa lolote linalotokea Zanzibar, baya au zuri?

Hebu msikilize Rais Dk. Shein: Mimi sipaswi kulaumiwa kwa kuchukuliwa viongozi wa Uamsho kushtakiwa Bara.

Anasema, “Nini watu kupelekwa kushtakiwa Tanzania Bara, viongozi wa ki Afrika wanapelekwa The Hague kushitakiwa, itakuwa Bara.”

The Hague, nchini Uholanzi, ndiko iliko Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ambako watawala na viongozi wa makundi ya kiharamia hushitakiwa.

Huko amepelekwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto, na wanasiasa wengine. Pia amepelekwa mtangazaji wa redio binafsi, Arap Sang.

Rais amesikia malalamiko ya umma. Makumi ya masheikh wa Zanzibar, wengi wao viongozi wa Jumuiya ya Uamsho, wako gerezani Bara wakikabiliwa na mashitaka ya ugaidi.

Masheikh hao walikamatwa majumbani kwao usiku na kusafirishwa hadi Dar es Salaam na kuwekwa vituoni. Walihojiwa kwa siku kadhaa. Hakuna aliyepewa nafasi ya kuwasiliana na familia yake. Wala serikali haikujulisha familia zao.

Baada ya wiki kadhaa, wakapelekwa Mahakama ya Kisutu chini ya ulinzi mkali na pingu mikononi. Wakahusishwa na ugaidi ambao chini ya Sheria ya Kudhibiti Ugaidi ya 2002, wanakosa dhamana.

Ndipo familia zao zilipoanza kuchangishana ili kupata usafiri wa kwenda Dar. Ni safari ngumu ya gharama kubwa.

Uchumi wa familia Zanzibar ni duni. Nchi haina uchumi wa maana, wananchi wanabaguliwa katika fursa za elimu na ajira kwa kuwa hawatii CCM.

Wanaotii CCM na wakubwa zake, wanaishi vizuri kwa sababu wanafadhiliwa. Vijana wao wanasaidiwa kusoma na kupata kazi.

Wasomi fulani serikalini walipata kunambia vijana waliowapitisha waajiriwe baada ya kufuzu usajili waliowafanyia mwaka 2012, waliachwa.

Nafasi zao walipewa wale ambao hata usaili hawakufanya. Ili kutomvunja moyo, akatafutiwa safari yenye posho. Mwenyewe alikuwa na mipango ya kusoma zaidi.

Suala la Masheikh wa Zanzibar kukamatwa na kusafirishwa Dar ambako kwa siku kadhaa – ikumbukwe sheria za nchi zinashurutisha mtu kupelekwa mahakamani ndani ya saa 24 tangu alipokamatwa – na kushitakiwa limechochea chuki kubwa dhidi ya serikali.

Baadhi ya familia zilituma mawakili kufungua shauri Mahakama Kuu Zanzibar, kutaka waihoji serikali kama kitendo cha kukamata watu Zanzibar na kuwashitaki Bara, tena kwa makosa wanayotuhumiwa kuyatenda wakiwa Zanzibar, ni halali kisheria.

Shauri hilo liliamuliwa na Jaji Mkusa Isaac Sepetu akisema hana uwezo wa kuingilia kesi iliyoko Mahakama ya Bara kwani haoni kifungu cha sheria kinachompa haki ya kufanya hivyo.

Alisema anavyoona si tatizo Jeshi la Polisi kukamata mtu Zanzibar na kumsafirisha Dar es Salaam ambako anafunguliwa mashitaka.

Mawakili wa masheikh hawakuridhika. Lakini pamoja na kuwapo fursa ya kukata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania, walisema hawaoni sababu ya kukata rufaa kwa kuwa “wanaona suala lenyewe limejaa siasa.”

Masheikh wengi katika kesi hiyo, ambao wanaendelea kuishi gerezani, ndio walewale walioshitakiwa Mahakama ya Zanzibar tangu 2012 na kukaa gereza la Kiinua Miguu, Kilimani, kwa zaidi ya mwaka mpaka walipopata dhamana baada ya kesi kufika Mahakama Kuu.

Mpaka sasa, kesi hiyo iliyoko mbele ya Jaji Fatma Hamid Mahmoud, haijaanza kusikilizwa. Mwendesha mashitaka mkuu wa serikali – Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) –hajaieleza mahakama ameandaa mashahidi wangapi.

Ndio kusema DPP hajajiandaa kuwasilisha ushahidi ili kuishawishi Mahakama iwatie hatiani watuhumiwa.

Mbele ya Mahakama ya Zanzibar, masheikh tisa na wasaidizi wao wanashitakiwa kwa kosa la kula njama kwa nia ya kutenda fujo na kusababisha uharibifu wa mali.

Nini maana yake? Ni kwamba wakati masheikh hao hawajasomewa ushahidi wa aina yoyote kwa kesi inayowakabili Mahakama ya Zanzibar, kwa zaidi ya miaka miwili sasa kesi ikiwa inaendelea na kuahirishwa, wanaumizwa kwa kesi ya makosa mazito zaidi kwenye Mahakama ya Tanzania Bara.

Akili ya kawaida ya mtu, atasema laiti kama serikali inayo kesi ya kweli iliyokusudiwa kuendeshwa kisheria, basi masheikh wangekuwa wanasubiri hukumu muda huu.

Ila sasa, kama Zanzibar wana kesi isiyosikilizwa, zaidi ya kutajwa na kuahirishwa, na hali hiyo ikiwa inaendelea kwa muda wote huo, lakini huku serikali ikiwa imewakamata watu haohao wakiwa Zanzibar, usiku wa manane, na kuwasafirisha kwa boti au kwa ndege, hadi Dar es Salaam, kuwaweka kizuizini kwa siku kadhaa, ndipo wanapelekwa mahakamani Kisutu, unaaminije kuwa lengo si kuwatesa na kuwazima?

Katika hali kama hiyo, tena unamsikia kiongozi mkubwa mwingine kama Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. Mohamed Gharib Bilali, ambaye sasa anakaimu urais wa Jamhuri, akisema hadharani “Uamsho ni kundi hatari linaloshirikiana na makundi ya Al Qaeda na Al Shabab,” mwananchi anatakiwa kufikiri nini hapo?

Matamshi yale ya Rais Dk. Shein kwamba hajali masheikh wa Zanzibar kukamatwa na kupelekwa Bara kushitakiwa, na haya ya Makamo wa Rais Jakaya Kikwete, yanajenga utawala bora, yanashajiisha utawala wa sheria kweli?

Matamshi ya wakubwa hawa tuseme yanashawishi wananchi, na hasa ndugu, marafiki na wanafunzi wa masheikh hao, kuiamini serikali na viongozi wake ni watu wema wenye uongozi mwema?

Kwamba serikali iliyowakamata masheikh na kuwatia gerezani katika mazingira hayo ya ujasusi huku wakitoa kauli za kebehi, za ovyo, inatenda haki?

Mbona athari za kauli zao zinaweza kuwa balaa? Ni kauli ambazo watu walio makini, ndani Tanzania au huko nje, wanaweza kuzitafsiri kwa uzito wake huohuo.

Hivi ni kweli si tatizo Mzanzibari kukamatwa Zanzibar na kupelekwa Bara kushitakiwa? Au Sheria ya Ugaidi mwisho Chumbe?

Basi serikali iseme “Tanzania ina ugaidi sasa.” Itakuwa imetenda haki na imewajibika. Ulimwengu utaelewa. Vinginevyo, si haki hata kidogo kutumia sheria, utawala ukakandamiza uhuru wa watu. Huko ni kuzivunja haki zao, na ndio uhalifu mkubwa unaowafikisha viongozi The Hague.

Chanzo: Mawio

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s