Tusiuvumilie uhuni aliofanyiwa Warioba

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alipovamiwa na genge la wahuni kabla ya kumalizika kwa kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwlaimu Nyerere.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alipovamiwa na genge la wahuni kabla ya kumalizika kwa kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwlaimu Nyerere.

Salim Said Salim

SERIKALI imeelezea “ kusikitishwa” kwake na vurugu alizofanyiwa Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba hivi karibuni katika Hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam 2  Novemba, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imekieleza kitendo hicho kama ni cha fedheha na kuwaeleza Watanzania kuwa kutokana na tukio lile serikali imeamua kupitia upya mpango wake wa ulinzi unaotolewa kwa viongozi wastaafu.

Balozi  Sefue amesema kuwa kitendo kile cha kihuni mbele ya hadhara ya watu waliokusanyika katika mdahalo kimeikera serikali kwa vile kimemvunjia heshima mzee Warioba.

Lakini licha ya kutolewa taarifa hiyo na Ikulu bado yapo masuala mengi yanayohitaji majibu sahihi juu ya namna ambavyo serikali yenyewe inavyomheshimu Jaji Warioba ambaye ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.

Kama nchi yetu imeamua kuwapuuza, kuwakejeli, kuwadharau na hata kuwakashifu viongozi wetu wastaafu ni vyema tukaelewa. Mtu haheshimiwi kwa maneno matamu bali pamoja na vitendo.

Haina ubishi kwamba mzee Warioba amegeuzwa katika siku za karibuni  kama tambara bovu ambalo kila mwenye uchafu wake huifutia. Tumeona kila mwenye kutaka kuonyesha utovu wa adabu wa kutukana na kukashifu mtu basi humgeukia mzee huyu, tena baya zaidi hata katika vyombo vya heshima kama Bunge.

Kwa bahati mbaya hata mawaziri wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wengine wakiwa amewazidi kiumri, elimu, urefu na hata kushika dhamana kubwa hapa nchini na nje nao wameingia katika uhuni huu wa kumtukana mzee huyu.

Mfano ni huyo waziri Hawa Ghasia, ambaye alifika hadi kufungua domo lake na kumwambia mzee Warioba akome.

Inawezekana kwamba malezi aliyopata huyu mama ni tofauti  na yale waliopata Watanzania wengine na ndiyo maana huyu Ghasia ameona kumwambia mtu mzima anyamaze ‘akome’ ni jambo la kawaida.

Lakini ukweli unabakia palepale kuwa katika lugha ya Kiswahili hili ni neno baya na halina heshima na halikutarajiwa kutamkwa na mtu aliyepata malezi mazuri.

Muungwana huona tabu hata kumwambia mtu mwingine muongo na badala yake humueleza “nadhani husemi kweli” au “naomba kutofautiana na maelezo yako”.

Naona ni vizuri siku zijazo watu wanaopewa nyadhifa za heshima kama mawaziri hapa nchini kupata mafunzo ya matumizi mazuri ya lugha ya Kiswahili na mtu mwenye adabu anatakiwa awe vipi mbele ya macho ya jamii

Baya zaidi pale huyo anayefungua mdomo wake kumwambia mtu akome uwa anafanya hivyo kwa mtu aliyemzidi umri na kuwa sawa au mkubwa zaidi kuliko baba yake.

Lakini kinachoshangaza ni kwamba Balozi Sefue hajatueleza hatua gani zimechukuliwa na serikali kuwashughulikia wahuni waliomvunjia heshima Jaji Warioba.

Watu waliofanya ule uhuni wameonekana mchana kweupe na hata zipo kanda na picha zinazoonyesha wazi wazi ni nani waliofanya vile.

Lakini wamenyamaziwa kimya kama vile walichokifanya ni jambo la kawaida na labda kinakwenda sambamba na kile ambacho CCM ukieleza kuwa watu wanaofanya mambo kama haya wanafaa kulindwa kwa vile ni “wenzetu”.

Lakini jingine linaloshangaza ni kwamba imechukua zaidi ya wiki moja kwa serikali kutoa taarifa hiyo kama vile palikuwa hapana uhakika kwamba kitendo kile ni cha kihuni na sio tu kilimvunjia heshima mzee Warioba, bali nchi nzima.

Wengi tulitarajia mara tu baada ya kufanyika uhuni ule wale waliofanya hivyo ambao wamesemekana kuwa ni mmoja wa kiongozi wa Jumuiya ya Vijana wa CCM angelichukuliwa hatua za kisheria.

Katika tukio kama hili tungetarajia hata viongozi wa juu wa serikali wangetoa tamko kukemea uhuni ule , lakini tulichokisikia ni baadhi yao kuomba yasiwakute kama yale yaliyomkuta Jaji Warioba.

Badala yake ni raia wa kawaida ndio waliosikika wakikemea jambo hilo na hata jeshi letu la Polisi halijatueleza limechukua hatua gani kuwawajibisha kisheria waliomfanyia uhuni ule Jaji Warioba.

Uhuni kama ule alipofanyiwa mzee wetu, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kwa kupigwa kibao tuliona kilichotokea.

Suala linaloulizwa na Watanzania wengi ni kwa nini hali imekuwa tofauti tukio kama lile alipofanyiwa mzee Warioba?

Hapa lipo jambo na linahitaji maelezo kwa vile kwa Watanzania wengi viongozi wote wastaafu wanastahili kuheshimiwa na wanaokubaliana naye kimawazo na wale wanaotafautiana naye bali kinaweza kuwapa nguvu wahuni wengine kufanya zaidi ya hayo.

Lakini kwa upande mwingine uhuni ule aliofanyiwa Jaji Warioba ni sawa na kusema tumeanza kuvuna matunda ya mbegu tulizopanda.

Ninasema hivi kwa sababu uhuni wa kuwatukana na kuwakashifu viongozi wastaafu umeshuhudiwa Zanzibar kwa muda mrefu.

Miongoni mwa viongozi waliotukanwa na kukashifiwa hivi karibuni ni Rais mstaafu wa Serikali ya Muungano, Benjamin Mkapa na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Tumeshuhudia hata kusambazwa mitaani na kwenye mitandao vipeperushi ambavyo vilikashifu viongozi wetu, lakini hapana hata mtu mmoja aliyekamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa kitendo hiki cha uhalifu.

Hata maskani baadhi ya maskani za CCM zimekuwa na ujasiri wa kuandika matangazo ya kuwatukana na kukashifu viongozi wastaafu na watu wengine. Lakini wote hawa hawakuguswa kama vile wapo juu ya sheria za nchi.

Yote tisa. Lililo muhimu ni kuelewa kuwa matokeo ya kuendelea kulea wahuni, wakiwemo wale wanaotumia vibaya nyadhifa zao kwa vile ni wabunge au mawaziri, ni mchezo wa hatari.

Kama viongozi wa sasa waliopo madarakani wataendelea kukaa kimya na kujifanya kama uhuni huu hawaoni wasije kushangaa na wao yakawakuta siku za usoni.

Tuombe Mungu tusifike huko wala kukaribia lakini ni vizuri tukachukua tahadhari mapema za kukomesha wahuni wanaovunjia heshima viongozi wetu na kutufedhehesha mbele ya jamii ya kimataifa.

Jamii bado inasubiri kuona hatua gani watachukuliwa waliomshambulia mzee Warioba. Kama kweli serikali haikufurahishwa na uhuni ule basi wale wahuni washughulikiwe ipasavyo kama sheria za nchi zinavyoelekeza.

Nimesema mara nyingi na zaidi kwa viongozi wa serikali na CCM kuwa waungwana na watu wenye mwelekeo wa utawala bora hulindana kwa mema na sio maovu.

Tuache kuoneana muhali kwa sababu za kijinga za utashi wa kisiasa. Kama tunataka wazee wetu katika nchi hii waheshimiwe na kuenziwa basi nasi tunapaswa kuwaheshimu na kuwaenzi, wakiwemo viongozi wetu wastaafu.

Tunataka kujenga taifa la watu wanaoelewana na kuvumiliana na sio kama la wahuni wanaotukanana, kukashifiana au kupigana.

Tumuombe Mungu atuepushe na wahuni wanaotaka kuipeleka nchi yetu kuwa jamii ya kihuni.

Chanzo: Tanzania Daima

 

Advertisements

One Reply to “Tusiuvumilie uhuni aliofanyiwa Warioba”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s