Keissy awavuruga tena Wabunge wa Zanzibar

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Mohamed Keissy
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Mohamed Keissy

NA MUHIBU SAID

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, jana alifanikiwa kudhibiti kuchafuka hali ya hewa bungeni baada ya wabunge kutoka Zanzibar kutaka ‘kumshughulikia’ Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy, (pichani) wakichukizwa na kauli yake waliyoitafsiri kuwa ni ya kuikejeli Zanzibar.

Keissy, ambaye mara kwa mara amekuwa akijikuta akiingia katika msuguano na wabunge kutoka Zanzibar, alitoa kauli hiyo akipinga kauli ya Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Rukia Kassim Ahmed, aliyoitafsiri kuwa ni ya kukejeli hatua ya Rais Jakaya Kikwete kwenda kutibiwa Marekani.

Rukia alitoa kauli hiyo katika mwongozo wa spika aliouomba bungeni jana chini ya kanuni ya Bunge ya 47 (1), (2) na (3).

Alisema kutokana na serikali kudaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) Sh. bilioni 102, hali imekuwa mbaya katika hospitali nchini, wagonjwa wanateseka, dawa hakuna, huku wabunge wakiendelea kupulizwa na viyoyozi bungeni na Rais Kikwete akiwa nje ya nchi kuchunguzwa afya yake.

“Kutokana na serikali kudaiwa Shilingi bilioni 102 na MSD, hali ya hospitali zetu ni mbaya sana, wagonjwa wameendelea kuteseka na maradhi, dawa hamna, wanawake wanakufa, watoto wanateseka, huku sisi waheshimiwa wabunge tukiendelea kukaa humu tukila viyoyozi. wa taarifa tulizo nazo mheshimiwa Rais yuko nje, kaenda kuchekiwa afya yake,” alisema Rukia.

Kutokana na hali hiyo, aliomba shughuli za jana za Bunge ziahirishwe ili kuwatendea haki Watanzania na kuokoa maisha yao kwa kujadili jambo hilo kwanza na kulipatia ufumbuzi kwa maslahi yao. Baada ya mwongozo huo wa Rukia kujibiwa na Ndugai, Keissy, alisimama na kusema Rukia hakupaswa kulinganisha hoja yake na Rais Kikwete kuwapo nje ya nchi kupatiwa matibabu na kuhoji kama alistahili kwenda kutibiwa Zanzibar.

Keissy alisema anawajua baadhi ya wabunge wa CUF, ambao wamekuwa wakienda mara kwa mara India kutibiwa na kusema iweje Rukia azungumzie habari za Rais Kikwete kwenda kutibiwa Marekani.

“Kulinganisha mheshimiwa Rais yuko nje kutibiwa, wabunge wangapi wa upande wa upinzani mara sita, kwa majina nawajua tena wa CUF wamekwenda India kutibiwa mara tatu mara nne, leo wanazungumza habari ya Rais kwenda kutibiwa Marekani, aende kutubiwa wapi, Zanzibar? Acheni mambo yenu hayo,” alisema Keissy.

Kauli ya Keissy iliwafanya wabunge kutoka Zanzibar kuhamaki na kuinuka na kutaka ‘kumshughulikia’. Hata hivyo, Ndugai kusimama na kuwasihi watulie na kuepuka kutoa kauli zinazoweza kuchafua hali ya hewa bungeni.

Wakati Ndugai akiendelea kuongea, Keissy alisimama na kuondoka katika ukumbi wa Bunge. Baadhi ya wabunge kutoka Zanzibar walimfuata Keissy, lakini wakashindwa kumfikia kutokana na kusindikizwa na askari wa Bunge.

Chanzo: The Guardian

One Reply to “Keissy awavuruga tena Wabunge wa Zanzibar”

  1. Mimi si kuona sababu ya Waheshimiwa wetu kuhamaki kwa mwenzao kutaja Zanzibar kama mahali ambapo Mheshimiwa Kikwete angeweza kutibiwa- Kwa hatua Zanzibar liyopiga kwani hawezi kutibu ugonjwa huu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s