Hivi huu mkanganyiko ni mimi tu au na ninyi mnauona?

Aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole
Aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole

Wahenga walisema anayeshindana na wakati atagonga ukuta.

Wiki hii napenda kuzungumzia suala ambalo mara zote watu wasio na nia njema hupenda kumrejea ndivyo sivyo rais wetu mpendwa na naona hii imekuwa desturi siku hizi. Mara kadhaa akizungumza, utaona siku zinazofuata watu wametohoa alichokisema mkuu wa nchi na mara nyingi huwa wametohoa ili kukidhi matakwa na masilahi yao. Hii siyo sawa.

Mkuu wa nchi alikwenda kwenye Bunge Maalumu akazungumza wengine wakadiriki kusema mkuu ameshatoa maelekezo, hata yeye mwenyewe alikuja kufafanua baadaye alichokifanya kwenye Bunge Maalumu na kwamba hakuwahi kutoa maelekezo.

Hata alipotutangazia kuwa na mchakato wa kupata Katiba Mpya, watu wale wenye hila hawakusita wakaenda mbali zaidi ya kutohoa maneno yake na hata kudiriki kumhoji na kuhoji uhalali wa uamuzi wake.

Unajua utovu wa nidhamu siyo suala la rika, ni suala la mtu binafsi au mtoto, kijana, mtu wa makamo au mzee. Kutohoa, kutafsiri na kupindisha kauli za mkuu wetu wa nchi ni kiwango kikubwa cha utovu wa nidhamu, hasa inakuwa mbaya zaidi pale ambapo anayefanya utovu wa nidhamu ni mtu wa makamo.

Hawa vijana ni matokeo ya namna mnavyotulea, mara nyingi sisi vijana hupenda kujinasibu na tabia na mienendo ya wale wanaotupa hamasa.

Kama wewe ni mwizi basi ujue wale vijana wako watakuwa wameanza ku-“develop” tabia za wizi. Kama wewe ni mtu mshari tu tena ngumi mkononi, basi huna haja ya kuhoji ukisikia watu wamepigwa ama wamerushiwa viti. Ujue kwamba, ile tabia yako inafanya kazi ndani ya wale vijana wako. Wale vijana ambao wanapata hamasa kutoka kwa watu wenye uchu ya madaraka kwa hakika utaona hata lugha zao mitandaoni ni za kibabe. Mara nyingi ni za matusi, vijana hawa huwa hawana simile, hasa mijadala inapokuwa imesheheni watu wanaoshindanisha nguvu za hoja. Punde wao hubadili kibao na kushindanisha hoja za nguvu na huwa hawana aibu. Nasikia hawa wanaweza hata kulipwa kufanya lolote. Hii ni shida tunaitengeneza leo na itakuja kutusumbua baadaye miaka kadhaa ijayo, Mwenyezi Mungu atupe umri na afya tutashuhudia.

Tofauti kati ya kampeni na elimu ya uraia

Nieleze bayana kwamba mchakato wa kuandika Katiba Mpya, unapaswa kuwa mchakato ambao wananchi wanashiriki kwa kiwango cha juu kabisa. Kimsingi wataalamu wa Katiba wanaainisha misingi mikubwa minne ambayo ni lazima izingatiwe pale nchi inapokuwa inaandika Katiba yake. (i)Public Participation yaani ushiriki wa watu, (ii) Inclusiveness (including gender equity) and representation yaani ujumuishi unaoheshimu dhana ya nafasi na usawa wa kijinsia pamoja na uwakilishi, (iii) Transparency yaani uwazi na (iv) ni National ownership yaani umiliki wa mchakato kitaifa.

Utagundua misingi hii niliyotaja inaruhusu wananchi kuendelea kujadiliana mpaka wakiwa kwenye mstari wa kwenda kupiga kura. Mijadala ni jambo la afya katika jamii yoyote ile iliyoendelea. Ni lazima watu wazungumze, wagonganishe mawazo yao kwa hoja na sababu na ni katika mchakato huu wa kujadiliana, ndipo uelewa mpana hujengwa na kusimikwa katika fikra za watu.

Watu wanapokuwa wameelimika basi mara zote huweza kufanya uamuzi sahihi. Hii ndiyo inaitwa elimu ya uraia juu ya mchakato wa kupata Katiba Mpya pamoja na maudhui yake. Tukizungumza maudhui ya mchakato huu ni pamoja na Katiba ya Mwaka 1977 inayotumika sasa, Rasimu Toleo la Awali, Rasimu Toleo la Pili pamoja na viambatisho vyote.

Watu wana haki ya kueleweshwa juu ya mambo haya. Mimi bibi yangu umri wake umekwenda sana, nadhani anafika miaka 100 na hajui kusoma wala kuandika, lakini haki ya kupiga kura anayo. Hivi, unadhani mimi nitamwacha Tumwihukage Semwenga au kama wajukuu tunavyomwita “Bibi Nundu”, aende akapige Kura ya Maoni pasina kuwa nimemsomesha?

Chanzo: Mwananchi

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s