Marufuku ya kampeni isiwe ya upande mmoja

Rais Jakaya Kikwete akiondoka kutoka katika mkutano wake na wazee Mjini Dodoma
Rais Jakaya Kikwete akiondoka kutoka katika mkutano wake na wazee Mjini Dodoma

Rais Jakaya Kikwete juzi alipiga marufuku vyama vya siasa na asasi za kiraia kufanya kampeni za kuhamasisha wananchi kuhusu Katiba Inayopendekezwa, akisema kufanya hivyo ni kuvunja Sheria ya Kura ya Maoni kwa kuwa muda wake haujafika. Akihutubia mkutano wake na watu wanaojipambanua kama ‘wazee wa Mkoa wa Dodoma’, Rais aliwahadharisha wananchi wasikubali kile alichokiita kudanganywa na watu wasioitakia mema nchi yetu.

Wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo, siku hiyo hiyo Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuacha kile alichokiita kutumia vibaya mchakato wa Katiba Inayopendekezwa kwa lengo la kuwagawa wananchi na kutishia amani na utulivu uliopo nchini. Alikuwa akizungumza na wananchi na viongozi wa CCM katika maadhimisho ya miaka minne ya kuwapo madarakani tangu aliposhinda urais mwaka 2000. Alisema kumeanza kujitokeza viashiria vya kuanza kuvuruga amani na utulivu uliopo hivi sasa kwa kisingizio cha mchakato wa Katiba Inayopendekezwa.

Sisi hatuna ugomvi hata kidogo na kauli hizo za viongozi hao, kwani ni wajibu wao kukemea au kutahadharisha wananchi pale wanapodhani kuna umuhimu wa kufanya hivyo. Lakini tumeshangazwa na hatua ya viongozi hao kufanya mambo ambayo ni tofauti na kauli zao za kukemea kampeni. Katika mikutano yao mjini Dodoma na Zanzibar juzi, viongozi hao walipiga kampeni kwa kutaka wananchi waunge mkono Katiba Inayopendekezwa. Rais Shein alisema Katiba Inayopendekezwa ni mkombozi wa wananchi wa Zanzibar na kudai imejibu hoja za malalamiko na kero za Muungano. Mjini Dodoma, Rais Kikwete aliisifia Katiba Inayopendekezwa, akisema uzuri wake hauhitaji kuambiwa na mtu kutokana na kuandikwa vizuri na kwa lugha rahisi, huku akiilinganisha na timu ya mpira iliyokamilika katika kila idara.

Hapa tumezungumzia tu kauli za kampeni walizozitoa juzi katika hafla tofauti mjini Dodoma na Zanzibar. Lakini mtu yeyote mwenye kumbukumbu nzuri atakumbuka kwamba viongozi hao, mawaziri na viongozi wa chama chao cha CCM wamekuwa wakitoa kauli nyingi za kuipigia kampeni Katiba hiyo inayopendekezwa. Tumeshuhudia wakifanya hivyo kila wanapopata fursa za kufanya ziara za kiserikali ama za kichama. Katika ziara zake wiki iliyopita katika mikoa ya Mwanza na Tabora, Rais Kikwete alifanya kampeni hizo na kuwataka wananchi wapige kura ya ‘ndiyo’ kwa Katiba hiyo inayopendekezwa, wakati Rais Shein alifanya hivyo mjini Zanzibar katika mikutano ya hadhara wiki mbili zilizopita, akiwa ameandamana na viongozi wa CCM na mawaziri waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Tumelazimika kutoa mifano hiyo kuonyesha kuwa, wakati vyama vya upinzani na asasi za kiraia zikipigwa marufuku kuwaeleza wananchi kuhusu maudhui yaliyomo katika Katiba Inayopendekezwa pamoja na Rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Ikulu ya Zanzibar na ya Serikali ya Muungano kwa muda mrefu zimekuwa zikijihusisha katika vitendo vya kupigia kampeni Katiba Inayopendekezwa.

Rasilimali na fedha nyingi za umma zinatumiwa katika kufanikisha mkakati huo, ambao pia unawahusisha baadhi ya wahariri na vyombo vya habari kadhaa. Tukio la mwishoni mwa wiki, ambapo wafuasi wa CCM walivuruga mdahalo wa Katiba na kumpiga Jaji Joseph Warioba wakati akiwasilisha mada kwenye mdahalo huo ni ujumbe tosha kwa kila mmoja wetu.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s