Jakaya na mafunzo ya akina Nyerere

warioba+px (1)Ahmed Rajab         Toleo la 378             5 Nov 2014

 

SIASA zina miujiza yake. Uongozi wa nchi nao una maajabu yake.

Hebu tuyatupie macho yaliyotokea wiki iliyopita Burkina Faso na yaliyomsababisha aliyekuwa Rais wa taifa hilo masikini Blaise Compaoré, mbabe wa miaka 27, ang’oke kwenye madaraka na akimbilie Côte d’Ivoire.

Yaliyotokea yalikuwa ni aina ya miujiza ya kisiasa. Tukijua kuna siku Compaoré ataporomoka, lakini hatukufikiria kuwa ataporomoka namna alivyoporomoka.

Mpaka mwanzoni mwa wiki iliyopita, Compaoré akihisi kwamba ataweza kufanya mazingaombwe ili aselelee kwenye madaraka. Kulikuwa kila dalili kwamba angefanikiwa.

Alikwishalisuka Bunge limkubalie Katiba ibadilishwe ili aweze kuendelea kutawala kwa muhula wanne baada ya kugombea uchaguzi mwingine ambao ungempatia ushindi.

Umma haukukubali tena kuchezwa shere. Ukasema “basi yanatosha.”  Wananchi wakamiminika mitaani na yakatokea yaliyotokea.

Jumapili iliyopita niliyatafakari ya Burkina Faso, nchi niliyowahi kulala chini ya anga yake na ninayozifuatilia sana siasa zake.

Nilipokuwa ninayatafakari hayo na huku naandika makala haya nilipata habari ya yaliyojiri siku hiyo ya Novemba 2 katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Nyerere uliokuwa ukijadili Katiba ya Tanzania iliyopendekezwa na Bunge la Katiba.

Uhuni uliofanywa kwenye mdahalo huo katika eneo la Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam, ulikuwa ni fedheha na aibu tupu.

Katika hujuma ile, wahuni (naambiwa baadhi yao ni viongozi ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi, UvCCM) waliuvamia mkutano alipokuwa anazungumza Jaji Joseph Warioba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba.

Walifyatua mabango walikokuwa wameyaficha, na mmoja wao, Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa CCM, Paul Makonda, alishiriki kikamilifu katika utovu huo wa adabu.

“Dhambi” aliyoifanya Warioba ni kueleza msimamo wa Nyerere kuhusu maadili, Azimio la Arusha na upinzani wake dhidi ya viongozi wenye kuhaulisha fedha nchi za nje.

Aliyoyasema yaliwakera baadhi ya wana CCM hao waliokuwapo na jibu lao likawa ni kuanzisha vurugu.

Uhuni kama huo siku hizi umekuwa ni tabia ya wanaCCM wenye vyeo vya juu na wakereketwa. Hakuna mwenye kuthubutu kuwakemea.

Fedheha hiyo ya Jumapili haikuwa fedheha ya chama hicho peke yake, bali pia ilikuwa aibu kwa Taifa zima na ilimpaka tope Mwenyekiti wa CCM, ambaye ndiye Rais wa nchi.

Chama cha CCM bado ndicho chama kikubwa cha siasa na chenye nguvu Tanzania. Hiki ni chama chenye historia ndefu kushinda vyama vyote nchini.  Kinajiweza kwakuwa na rasilmali kubwa ya fedha iliyokiwezesha kushika hatamu za utawala kwa miongo mingi.

Hivi sasa wananchi wana shauku kubwa ya kutaka Katiba yenye maoni yao. Hadi sasa kinachowazuia wasiipate Katiba aina hiyo ni njama za CCM. Wakati huohuo mabishano yamepamba moto baina ya CCM na Umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA) na baina ya CCM na wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Katiba.

Mazingira yote haya hayaashirii hali njema ya utulivu wa kisiasa nchini. Wanaochungulia nyuma ya pazia la siasa za Tanzania hawaoni kitu ila vimurimuri.

Wachunguzi waliofuatilia kwa makini yaliyozuka katika Bunge la Katiba na jinsi rasimu ya Katiba iliyopendekezwa ilivyotungwa, wameingiwa na hofu juu ya mustakbali wa demokrasia Tanzania. Wanachelea kwamba katika muktadha huu siasa zitaathiriwa kwa muda mrefu na matukio haya ya Katiba mpya.

Maandalizi ya Katiba hiyo yamekumbwa na mushkili. Baada ya mchakato wa Katiba kutekwa nyara na wajumbe wa CCM waliokuwa katika Bunge la Katiba, kuna hoja tatu zilizoibuka — ya kisiasa, ya kisheria na ya kimaadili.

Wenye kutoa hoja ya kisiasa wanasema kuwa Katiba ya nchi lazima iwakilishe maoni ya wengi wa wananchi. Hoja hiyo inapingwa na CCM, chama chenye kujiona kwamba ndicho pekee chenye kuyawakilisha maoni hayo.

Wenye hoja ya kisheria wanahoji kuwa taasisi za kusimamia kura ya maoni kuhusu Katiba haziaminiki kwa vile hazina uwazi na zinakipendelea chama cha CCM, hasa Zanzibar.

Wenye kutoa hoja za kimaadili wanahoji kwamba Katiba iliyopendekezwa haina uhalali kwa sababu ilipatikana kwa ghilba na udanganyifu.

Kwa sasa kimya kimetanda kila pembe ya nchi; kwa jumla wananchi bado hawakuanza kupiga kelele kwa kishindo.  Wamekaa kama walioduwaa mithili ya watu walioapizwa na kenge. Kwa kawaida kimya kama hiki huwa hakidumu kwa muda mrefu.

Ghafla, bila ya kutarajiwa, wananchi husema “basi yanatosha” na hapo huanza kuripuka na wanapoanza kelele zao huwa hapakaliki. Hutokea kama yaliyotokea Burkina Faso wiki iliyopita.

Kwa kiwango kikubwa matatizo ya Tanzania juu ya Katiba iliyopendekezwa yanatokana na watawala, hususan, Rais Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM.

Matamshi yake wakati wa ufunguzi wa Bunge la Katiba na ahadi kadhaa alizozitoa na kuzivunja kuhusu mchakato wa Katiba, zimechangia kuwafanya wananchi waitoe maanani rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Bunge la Katiba.

Uongozi wa sasa wa CCM una mtizamo na fikra finyu. Chambilecho Mwenyekiti Mao aliyekuwa akiiongoza China uongozi wa CCM ya leo umekaa kama chura aliye chini kisimani.

Akiangalia juu hufikiri kuwa ukubwa wa mbingu ni sawa na sehemu ya wazi ya juu ya kisima. Mpaka atapotoka nje ya kisima ndipo atapokuwa na mtazamo mwingine kabisa.

Huo mtizamo finyu ndio unaomfanya Jakaya Kikwete aonekane kuwa katika mambo ya kuongoza nchi na maadili ya uongozi, yeye na Mwalimu Julius Nyerere ni kama mbingu na ardhi.

Silaha kubwa aliyokuwa akiitumia Nyerere ilikuwa ni ulimi wake. Si mkuki, si bunduki. Bali ulimi. Lakini ulimi wake haukuwa na sumu kama ule wa Rais Michael Sata wa Zambia aliyefariki London Jumanne iliyopita. Wa Sata ulikuwa mkali uliojaa usafihi. Wa Nyerere ulikuwa wa kuuma na kupuliza.

Nyerere aliyatumia maneno kujengea msingi wake wa kisiasa. Namna alivyokuwa akizungumza, namna maneno yalivyokuwa yakimtiririka, ilikuwa kama alimeza kamusi.

Nyerere alikuwa mfaume-msomi. Alikuwa mtawala aliyekuwa akifikiri. Alijaribu kuwashawishi wanananchi wenzake kwa hotuba zake za kusisimua. Aliwashawishi na wengi walishawishika. Walikuwa kama njiwa waliopigwa na bumbuazi walipokuwa wakimsikiliza akiwa jukwaani.

Kuna waliojidai tu kushawishika na kuna waliozipinga fikra zake, wengi wao kisirisiri.  Na baadhi ya hawa ndio wenye kuiongoza CCM ya leo.

Nyerere aliimudu kazi ya kuushawishi umma kwa sababu akiziamini fikira zake. Akijiamini mwenyewe, ingawa kujiamini kwake kulimfanya awe na ule ujeuri ambao aghalabu wasomi huwa nao. Hakuweza kuwavumilia wale aliowaona kuwa wapumbavu.

Na Nyerere akiripuka kama alipokasirika pale dikteta wa Uganda Idi Amin aliposema kuwa jinsi alivyokuwa akimpenda lau angelikuwa mwanamke angemuoa. Ufedhuli kama huo ukimkera. Matamshi hayo yalimfanya Nyerere amuone Amin kuwa ni sefle.

Nyerere alikuwa na mabaya yake lakini si yeye wala si wasaidizi wake waliothubutu kufanya mambo ya kihuni kama yafanywayo na wanaCCM wa leo.

Asingeliuvumilia uhuni na utovu wa adabu kama tunaoushuhudia siku hizi miongoni mwa baadhi ya viongozi na wakereketwa wa CCM wa Tanganyika na Zanzibar.

Alipoona kwamba sera zake hazikuleta maendeleo aliyoyatarajia hatimaye Nyerere ilimbidi akiri kwamba hazikufanikiwa. Kama sera zake za Ujamaa zilishindikana basi zilishindwa huku mwenyewe Nyerere akibakia na heshima yake.

Sera hizo hazikufanikiwa kwa sababu ama utekelezwaji wake ulikwama katika tope za urasimu au kwa sababu wale waliokuwa na dhamana ya kuzitekeleza walizitekeleza vibaya. Inaweza kuwa baadhi ya watekelezaji walifanya kusudi kuzitekeleza vibaya kwa sababu wao wenyewe walikuwa hawaziamini kwa dhati.

Kuna uwezekano mwingine pia ambao wapenzi wa Nyerere hawataki kamwe kuusikia: kwamba sera hizo hazikuweza kutekelezwa kwa sababu zilikuwa hazitekelezeki.  Hazikuweza kusimama kwa sababu hazikuwa na miguu imara. Hata hivyo, katika uongozi, Nyerere alikuwa imara. Hakuwa na ugeugeu. Hilo ni funzo kubwa la Nyerere.

Kuna viongozi wengine wa dunia ambao wana mafunzo mazuri pia.  Mfano ni Rais wa Bolivia Evo Morales na rafiki yake Mahmoud Ahmadinejad aliyekuwa Rais wa sita wa Iran.

Morales alinishangaza majuzi alipochaguliwa Rais kwa muhula wake wa mwisho aliposema kwamba atapoumaliza muda wake wa Urais atafungua mkahawa.

Alisema akiingia katika biashara hiyo atachuma fedha nyingi kushinda mshahara anaoupata akiwa Rais kwani wateja watamiminika kwa mkururo mkahawani kwake wakitaka kupiga naye picha.

“Fikiria watakuwaje watapohudumiwa na Rais mstaafu,” alisema huku akitabasamu.

Ni nadra siku hizi kumpata kiongozi kama Morales. Huyu ni kiongozi aliye kipenzi cha umma. Ni kiongozi asiye na mbwembe, asiye na makuu katika maisha yake. Naikumbuka picha aliyopiga miaka michache iliyopita katika karamu ya kitaifa aliyoandaliwa rasmi Teheran, Iran, wakati wa enzi za Ahmadinejad. Picha inawaonyesha viongozi hao wawili wakiwa wameketi chini juu ya zulia wakipiga msosi.

Ahmadinejad naye hakuwa na mbwembwe. Alipokuwa Rais akiishi kama wanavyoishi watu wa kawaida.  Hakuwa na makuu katika mavazi au kwa namna alivyokuwa akijiweka. Picha aliyopigwa uwanja wa ndege wa Teheran Agosti 16, 2011 alipokwenda kumpokea Morales inaonyesha jaketi alilovaa Ahmadinejad limefumka kwapani.

Viongozi hao hawakushughulishwa na masuti mazuri ya kuwafanya wao wapendeze. Walishughulishwa na jitihada za kuzifanya hali za maisha za wananchi wa kawaida nchini mwao ziwapendeze hao wenzao hususan wale wa matabaka ya chini.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s