Wamevamia karamu si yao, wakafanya fujo

Jaji Warioba wakati akitolewa kwenye ukumbi baada ya kutokea fujo zinazoshutumiwa kufanywa na baadhi ya vijana waliojipanga kuharibu Kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Jaji Warioba wakati akitolewa kwenye ukumbi baada ya kutokea fujo zinazoshutumiwa kufanywa na baadhi ya vijana walioongozwa na Paul Makonda waliojipanga kuharibu Kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.

Na Ally Saleh

Matukio mawili makubwa yametokea nchini wiki hii katika uwanja wa siasa na yote yakiwa mjini Dar es Salaam, na kwa fikra zangu yote mawili yatakuwa yametikisa rubaa ya kisiasa.
Pia matukio hayo yanatoa mafunzo makubwa kwa nchi, ijapokuwa yanasifa mbali mbali ambapo moja ni la maendeleo makubwa na jengine ni la aibu kubwa. Lakini kwa kuwa mtu lake halimtapishi, kama Waswahili wanavyosema tumelipokea, ila tusikubali kurudia tena.

Tukio jema ni lile la Oktoba 31 ambapo Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) kilionyesha umma kuwa kumbe Watanzania wanaweza kufikiri nje ya boksi, na kwamba ukongwe wa chama si kuwa ni miliki wa fikra na ubunifu.

Nchi hii zama na zama imeshika mfumo wa uanachama kwa njia ya kadi na CHADEMA wamekuja na ubunifu wa wanachama kwa njia ya eletroniki yaani e-members ambapo tena zile zama za kwenda mafunzo ya itikadi, sijui ule kiapo na ahadi za uwanachama umepitwa na wakati.

Pia wakaja na ubunifu mwengine wa kuchangisha kwa njia ya mtandao na hivyo kuzidisha uwezekano wa chama kuwa cha wananchi ambapo wananchi hao kwa sasa million 29 katika Watanzania million 45 wana simu za mkononi.

Chadema inajigamba kuwa ina wanachama 5,000 kama kila mwanachama atajikusuru angalau atoe shs 500 kwa mwezi basi tunazungumzia mabilioni ambao CHADEMA itakusanya na sio kukamuana kila siku. Na bila ya shaka ni mtaji mzuri kuelekea Uchaguzi Mkuu lakini kwanza Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Vile vile CHADEMA imetuonyesha inaweza kujenga msingi mzuri wa wanachama kwa njia hio ya mtandao na ambao wanachama hao kwa kutumia nyenzo hiyo, chama kinaweza kuwasiliana na wanachama wake kwa jumbe ndogo ndogo za kisera, kikampeni na maelekezo mengine.

Bila ya shaka hili litageuza uwanja wa siasa wa Tanzania na tunatarajia vyama vyengine navyo vivute fikra na kuja na mbinu nyengine kutumia teknolojia kutandika siasa za vitendo na shirikishi, maana pia wakati sio tena huu wa kila siku kuitisha mikutano ya hadhara ambayo ina athari katika uzalishaji na ni gharama kwa upande wa kiusalama.

Hilo ni la Ijumaa lakini, la Jumapili la Ubongo Plaza lilikuwa ni la aibu na linafaa likemewe kwa nguvu zote na waliohusika walaaniwe na wenye nafasi za kuchaguliwa kama kiongozi wa juu wa Umoja wa Vijana wa CCM, kupitia mtandao wa Chipukizi, Paul Makonda ajiuzulu kwa aibu.

Tukio hilo ni lile la mdahalo wa kupitia Katiba Inayopendekezwa ambayo uliandaliwa na Mfuko wa Mwalimu Nyerere na kuhudhuriwa na waliokuwa Wajumbe wa Tume ya Warioba na ambao ndio waliokuwa wasemaji katika hafla hiyo.

Mdahalo huo ulikuwa ukienda vyema kwa kusikiliza hoja za aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji kuhusu mlinganisho wa Rasimu ya Pili na Katiba Inayopendekezwa hadi pale kundi la vijana lilipoinuka na mabango kadhaa ambayo kimantiki yalikuwa yanapingana na yaliokuwa yakisemwa na Warioba.

Moja wapo lilisema “ Tumeipokea na tunaikubali Katiba Inayopendekezwa,” na badala ya kunyanyua tu mabango bali wabebaji wa mabango hayo wakaranda kwenye ukumbi na kufikia hatua hata ya kuimba “CCM, CCM,CCM” Yaani kwa maana nyengine wamevamia karamu si yao kisha wakafanya fujo.

Tuseme ni sawa wao ni Watanzania na walikuwa na haki ya kuhudhuria. Au tuseme ni sawa walikuwa na haki ya kuonyesha hisia zao. Lakini jee tuna utamaduni huo? Tunaweza kuwa na ustahamilivu kama huo? Jee leo kwa wenzao kesho kwao haitakuwa mkuki kwa nguruwe?

Tumeanza hivi kwa mdahalo wa mwanzo wa Katiba Inayopendekezwa, jee si kuanza kwa mguu wa kushoto wakati tuna safari refu? Kama siku ya mwanzo kuna watu wamekosa ustahamilivu na kuingia na kachumbari na chatine katika karamu ya watu, jee katika karamu zao watastahamili au watalindwa na vikosi vya FFU na kutumia dola kichama?

Na kama kiongozi wa kitaifa kama Paul Makonda, ambaye alikuwepo hadhirani na kuhusika kwa kiasi na mkasa uliotokea, kama alikuwa akijua au hakuhusika katika kupanga, ameshiriki katika kitendo cha aibu kabisa na kwa kipimo kikubwa hawezi wala hafai na hatoshi katika nafasi yake.

Ni vyama UVCCM ikamtizama mpya kiongozi huyu na CCM yenyewe ikatizama kiongozi huyu kwa sababu si rahisi katika hili taasisi hizo mbili kujivua dhamana na kama zitajivua maana yake wamkane Makonda na kukanwa kwake ni kuvuliwa madaraka.

Wengi wetu tumekuwa tukisema kuwa ujenzi wa katika ni maridhiano na tukio hilo limeanza kupanda mbegu mbovu za kukosa maridhiano na kupelekea ujumbe mb aya kwa umma kuwa kumbe ni vurugu na fujo kuelekea Kura ya Maoni.

Tungependa tusikie kauli kali na ya kukemea ya Serikali. Rasimu Inayopendekezwa sio tamko la Mungu ambalo haliwezi kukosolewa au limekamilika kama tunavyooamini kwa vitabu vitakatifu. Katiba ni yetu sote na kila mmoja wetu ana haki kusema anavyoaamini.

Makonda na wenziwe kama alihusika kupanga wangeweza kusikiliza uongo wa Warioba na wenziwe na kisha kutoa maoni yao au kujuburi hoja zao. Au wangesikiliza kisha kuandaa kongomano lao na kusema na kuukosoa uongo wa Warioba na wenziwe badala ya matendo ya kuwashushia hadhi.

Hili limenipa fikra niwaze. Kumbe si hoja kuwa mkongwe wa umri kwa busara, wala si hoja kuwa kijana kuwa na muono. Na hili linanipa mawazo kuwa haya yasipozingatiwa msemo wa Tanzania ni kisiwa cha amani utamalizika, maana hata Burkina Faso waliamini hivyo.

Chanzo: Mtanzania

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s