Makonda ajipalia makaa

Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Paul Makonda anayeshutumiwa kuchafua hali ya hewa kwenye kongamano la katiba
Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Paul Makonda anayeshutumiwa kuchafua hali ya hewa kwenye kongamano la katiba

SIKU moja baada ya Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Paul Makonda kuongoza genge la wahuni kuvuruga mdahalo wa katiba mpya uliyoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, chama chake na Jeshi la Polisi wamekwepa kuzungumzia tukio hilo, huku Rais Jakaya Kikwete akipiga kijemba kiana.

Makonda na vijana wenzake takribani 15, walizusha vurugu hizo juzi wakati Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, akihitimisha hotuba yake na hivyo mdahalo huo kuhairishwa, ingawa hadi sasa jeshi la polisi halijachukua hatua yoyote kwa watuhumiwa.

Jana, Makonda aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo na kukana kumpiga Jaji Warioba huku akijitetea kwamba alikuwa akijaribu kumkinga asidhuriwe na wafanya fujo hao.

Wakati Makonda akijaribu kutoa utetezi usiokuwa na mashiko, Chama Cha Mapinuzi (CCM) Taifa, kimeshikwa na kigugumizi kulizungumzia tukio hilo, ambapo Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alidai yupo nje ya nchi na hivyo hana taarifa za kuwepo kwa vurugu hizo.

JK na Warioba

Naye Rais Kikwete katika kuipigia debe katiba mpya inayopendekezwa ambayo inapingwa na Tume ya Warioba, alitamba kwamba haoni aibu kuipigia kampeni katiba hiyo huku akikejeli kiana, kauli ambayo inaweza kutafsiriwa kama ilimlenga Jaji Warioba.

Bila kumtaja kwa jina, Rais Kikwete wakati akiwahutubia wakurungezi wa Taasisi za kuzuia na kupambana na rushwa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) katika mkutano uliyofanyika jijini Mwanza jana, alisema kuwa; “sioni haya kuitetea katiba mpya inayopendekezwa kama yule wa jana alivyofanya”.

Rais Kikwete ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa 12 wa kila mwaka wa taasisi hizo (SAFAC), uliohudhuriwa na wajumbe toka Tanzania, Botswana, Lesotho, Malawi, Msumbiji na Namibia, huku nchi za Angola, Zimbabwe, Afrika Kusini na Zambia zikiwa hazijawakilishwa.

Licha ya hotuba yote kuwa ya Kiingereza, ilipofika sehemu inayohusu katiba mpya, Kikwete alisema “Sioni haya kuipigia kampeni katiba mpya iliyopendekezwa ipite, mimi sio kama yule wa jana”.

Kauli ya Kikwete imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Jaji Warioba kufanyiwa vurugu na kudhalilishwa na vijana wa CCM wakiongozwa na Makonda katika mdahalo uliyoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere juzi.

Licha ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Joseph Butiku kuitaka serikali iwachukulie hatua wahusika akisema wameonekana na kutambulika, jeshi la polisi limeonekana kupiga chenga kuzungumzia tukio hilo, ambapo Kamishna wa Kanda Maaalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtupia mpira Kamanda wa Kinondoni, Camilius Wambura ambaye kwa siku nzima ya jana hakupokea simu yake ya kiganjani.

Makonda alivyojitetea

Akizungumza na waandishi wa habari, Makonda alijichanganya juu ya utetezi wake akisema kuwa alikuwa ni miongoni mwa watu waliompa ulinzi Jaji Warioba ili asidhuriwe na vijana waliotambuliwa kuwa wanatoka katika jumuiya ya chama hicho.

Makonda alijichanganya wakati akijibu swali la kwanini atajwe katika vurugu hizo, ambapo alisema kuwa wakati vurugu zilipoanza alimkibilia Amon Mpanju ambaye ni mlemavu wa macho na kwenda kumuhifadhi kabla ya kumfuata mwandishi wa habari wa BBC, Anord Kayanda aliyekuwa amejeruhiwa kwa kiti kichwani.

Alisema alitoa msaada huo baada ya kuombwa na Jaji Warioba na Joseph Butiku, ahakikishe vurugu hazitokei na Mpanju hadhuriwi katika mazingira aliyokuwa.

“Niliongea na Jaji Warioba kisha Butiku wakanieleza nihakikishe vurugu hazitokei na hali ilipokuwa ngumu nikamueleza Mzee Warioba aondoke kwa kuwa hali imekuwa mbaya na nikamshika mkono kumuondoa na huu ulikuwa msaada wangu kwa watu watatu tofauti katika muda ule wa vurugu,”alisema Makonda ingawa maelezo yake yanatofautiana na picha zilizopigwa akidai zimefanyiwa ufundi.

CHADEMA, CUF

Akizungumza tukio hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), Patrobas Katambi, alisema kitendo kilichofanywa na UVCCM ni makakati wa kutumia nguvu ili katiba pendekezwa isijadiliwe na wananchi.

Alisema kilichofanywa ni udhalilishaji kwani kitendo cha kuwapiga wazee kinawafanya wawe mashakani muda wote wanapowaona vijana.

Alisema tukio la juzi linaonyesha nchi kutokuwa na amani na viongozi wanaoshabikia amani kuvunjika wameshaanza kujidhihirisha kwa matendo yao.

Naye Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Halima Mdee, amelaani kitendo hicho cha vijana kumfanyia vurugu Jaji Warioba akisema ni janja ya CCM kujaribu kuzuia wananchi kuujua ukweli wa mapungufu yaliyo kwenye katiba pendekezwa.

Alisema kuwa wanawake wa CHADEMA wanapinga utovu wa nidhamu ulioonyeshwa na Makonda kwa vurugu walizofanya na kuhatarisha usalama wa washiriki wa mdahalo wakiwemo viongozi hao wastaafu, jambo lililosababisha mdahalo kuahirishwa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Magdalena Sakaya alisema kuwa CCM inalifikisha taifa pabaya kutokana na kitendo chake cha kuandaa vurugu na kwamba vijana waliofanya jambo hilo walijiamini kwa kuwa wanawajua waliowatuma.

Alisema suala la mdahalo lilikuwa ni kuwapa wananchi elimu juu ya katiba pendekezwa na kwamba watu waliokaa nchi nzima kuangalia mdahalo huo walikatishwa kutokana na udikteta wa CCM kutaka kuongoza milele.

“Tumechoka kuongozwa na CCM kidikteta na kuna wasiwasi mkubwa wanaweza kuwaua hao wazee kutokana na kutapa tapa kwao baada ya kuona wananchi wanahitaji mabadiliko kama mvua ya mafuriko,”alisema.

Aliongeza kuwa CCM walijua wamefanikiwa baada ya kupitisha rasimu yao kwa shangwe na sherehe, kumbe hakuna lolote ndio kwanza wamechochea moto wa kuendelea kwa midahalo mbalimbali hadi kieleweke.

Wanaharakati, Wasomi

Mtandao wa Watezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umetaka serikali kutolifumbia macho suala hilo na kwamba ihakikishe watuhumiwa wanafikishwa kwenye mikono ya sheria.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, ilisema inapaswa ieleweke kwamba katiba ni suala la kitaifa na wala si la kikundi kimoja, hivyo kitendo chochote cha kutaka kuwanyamazisha watanzania wasiseme lolote kuhusu katiba pendekezwa ni dalili za kutaka kuipelekea nchi kwenye machafuko.

Alisema wananchi ama kundi lolote la kijamii lina haki kuendesha midahalo na kuelimishana kuhusu katiba pendekezwa kwa kuangalia kama imekidhi matarajio ya Watanzania.

Ikumbukwe kuwa, katika karne hii Tanzania inatakiwa kutengeneza katiba itakayokua ya mfano ulimwenguni kwani nchi sasa haipo kwenye mfumo wa chama kimoja kama ilivyotengenezwa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Naye msemaji wa Kitengo cha Lugha cha Umoja wa Afrika kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Aldin Mutembei, amesema vurugu zilizotokea juzi, zimemsikitisha kwani matokeo yake yatakuwa ni mabaya.

Prof. Matembei alisema vurugu zilizotokea ni vema zikaachwa na zisijirudie tena kwani zinaweza kusababisha madhara kwa nchi ambayo ni ya amani.

“Ni jambo la kusikitisha sana na kulikemea, tumekilaani kitendo hicho na tunaomba kisijirudie tena, kwani Tanzania ni nchi ya amani, hivyo basi iendelee kuwa na amani,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Veteran wa CCM Mkoa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Dar es Salaam, Abdallah Wazo, alisema azimio la Arusha linayumba kwasababu siasa safi imeanza kuingia dosari, hivyo amewaomba vijana wafuate nyayo za waasisi, na ambao wamepata madaraka wawe viongozi bora na sio kiongozi mwenye tamaa za fedha.

 Chanzo: Tanzania Daima
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s