Wapinzani waseme ‘haya twende’

umoja na mshikamano wa vyama vya siasa katika kusonga mbele kimaendeleo ni muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa hili la Tanzania
umoja na mshikamano wa vyama vya siasa katika kusonga mbele kimaendeleo ni muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa hili la Tanzania

Salim Said Salim

MTOTO anapozaliwa hutoa kilio na anapochelewa kufanya hivyo huonekana kuwa sio jambo la kawaida na kuna kuwepo wasi wasi juu ya hali ya mtoto huyo. Inapotokea mtoto hajatoa hicho kilio, mzazi kama anajiweza wakati huo au mtu yeyote yule aliyekuwa karibu humpiga vikofi vidogo mtoto huyo kwenye makalio au mapaja ili alie.

Watu wanaoelewa masuala haya kwa undani wanasema hicho kilio cha kwanza cha mtoto mchanga kina umuhimu wake kwa maisha.

Umuhimu huo ni wa kuonyesha kiumbe kilichokuja duniani , baada ya kuwa na uhakika wa chakula, maji, malazi na usalama tumboni kwa mama, ameonyesha kuelewa amekuja katika dunia yenye matatizo ya chakula, malazi na usalama tofauti na alipokuwa tumboni kwa mama.

Hili ni somo muhimu  sana kwa maisha ya binadamu. Baada ya hapo watu husoma kupitia kwenye matamshi, wanayoyaona au maandishi ya ubaoni au kwenye vitabu wanapokuwa shule au katika madrasa.

Baadaye yapo mafunzo ya aina mbali mbali ya maisha kwa nyakati tafauti. Haya ni pamoja na hayo yanayoitwa maandishi ya ukutani ambayo hutarajiwa kutoa ujumbe maalum kwa mtu au jamii, kama wanaohusika wanataka kujifunza na kuukubali ukweli au hali halisi iliyopo wakati ule.

Siku hizi watu wengi uandika habari au kutoa maelezo ya kumtaka mtu  akubali kusoma “ maandishi ya ukutani” (the writings on the wall). Lakini kwa bahati mbaya baadhi ya watu hutumia lugha hii bila ya kujua maana halisi ya maneno haya, makusudio yake au chimbuko lake.

Kweli maandishi ya ukutani ni yenye historia ndefu na tokea hapo mwanzo yalipochomoza yamekuwa yakitoa ujumbe wenye umuhimu mkubwa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu, maandishi ya ukutani ni ujumbe unaonyesha ishara ya kutokea jambo baya au sio la kufurahisha  kama haijachukuliwa tahadhari mapema.

Chanzo chake ni maandishi katika Biblia kongwe 5:1–31  (Old Testament) yalioandikwa na Danieli yanayoelezea kilichotokea katika karamu ya kunywa mvinyo iliyoandaliwa na mfalme Belshazzar wa Babylon katika karne ya 6.

Siku ile yalionekana maandishi kwenye ukuta ambayo yalikuwa yanamuonya mfalme. Wachawi na washauri wa mfalme walipuuza na kucheka, lakini kama yalivyoeleza maandishi haikuchukua muda kwa yule mfalme kuuawa.

Siku hizi msemo huu wa  kumtaka mtu asome “maandishi ya ukutani” hutumika sana kuwaonya watu, hasa viongozi, juu ya athari na hatari za kukataa kusoma maandshi hayo ya ukutani, yaani kuikubali hali halisi iliopo.

Hapa kwetu siku hizi viongozi wetu wengi wa serikali na hasa wale wa CCM wanaonekana sio tu hawataki kusoma maandishi ya ukutani, bali wanayafumbia macho, wanajifunga vitambaa vyeusi ili waone kiza na hata kutia pamba masikioni ili wakisomewa wasisikie.

Matokeo yake ni kuwa mara nyingi kinachotakiwa na umma kwa njia mbali mbali, ikiwa pamoja na kuweka maandishi ukutani hupuuzwa na kutupiliwa mbali.

Miongoni mwa mifano ya kuonyesha viongozi wa CCM wanakataa kusoma maandishi ya ukutani ni ya wingi wanaotaka mfumo wa Muungano wa serikali tatu kupitia maoni waliyatoa wananchi kupitia Tume ya Jaji Warioba. Hii ni hatari kubwa, sio kwao tu viongozi wa CCM bali pia kwa nchi.

Kwa kweli mchezo unaofanywa na CCM wa kukataa kusoma maandishi ya ukutani, yaani kukubali kinachotakiwa na kuamuliwa na wengi, ni kuisaliti demokrasia. Hata wakati wa mfumo wa chama kimoja uamuzi wa wengi, kama katika uchaguzi, ambapo walikuwepo wagombea wawili wa chama kimoja uamuzi wa wengi uliheshimiwa.

Tukitafari mwenendo wa CCM tunaouona hivi sasa wa kubadili maamuzi ya wengi kwa visingizo vya aina kwa aina kama “maslahi ya umma” , kuendeleza “mshikamano” , kutumia “utaratibu tuliojiwekea” au “kuendeleza amani na tulivu” tunachokiona ni kuendeleza nchini mvutano ambao hatima yake inaweza kuwa mbaya.

Ni vizuri tukaheshimu wosia wa wahenga wa “ wengi wape” badala ya wachache kung’ang’ania wao ndio wenye haki na kulazimisha mambo.

Kwa CCM ambayo ilizaliwa kutokana na vyama vilivyoleta uhuru (Tanganyika) na ASP kufanya Mapinduzi isiwe (Zanzibar). Mambo yanabadilika na anayekataa mageuzi ni mchawi.

Tuangalie hali ilivyokuwa katika nchi nyingi, pamoja na za majirani zetu ambapo vyama vilivyoleta ukombozi sasa vimetoweka au kutokuwa na nguvu kutokana na wananchi kupoteza imani kwa vyama hivyo.

Hata Rais wa Zanzibar, mzee Abeid Karume, alisema ukiona koti linakubana au  limechakaa unalitupa na kutafuta jingine. Hivi ndivyo wananchi wengi siku hizi wanavyoiona CCM na ndio maana wanataka kuiambia kwaheri wa salam na amani.

Maandishi yaliopo ukutani  hivi sasa yanaonyesha wazi kwamba kwa hali ilivyo CCM hivi sasa haina mpya. Wimbi la kutaka mageuzi linalovuma nchini  halizuiliki na kujaribu kuliwekea vikwazo  ni sawa sawa na kuzuia upepo usivume.

Kila zama zina mambo yake na hizi ni zama za wananchi kutaka mageuzi nchini na hili limeonekana katika mchakato wa kutafuta maoni ya katiba.

Kama mtoto mchanga anavyobadilika na baadaye akawa kikongwe asiyejiweza na kutegemea kusaidiwa  hivyo hivyo huwa kwa vyama vya siasa. Kuukataa ukweli huo ndio huko kunakoitwa kukataa kusoma maandishi ya ukutani.

Hivi saa Katibu Mkuu wa CCM, Ibrahim Kinana anazunguka nchi nzima kutaka kuipa CCM uhai mpya, lakini badala ya kukijenga chama ndio anazidi kubomoa kwa kutoa amri moja baada nyingine, kama vile anaongoza gwaride la kijeshi.

Kinana, akishavaa magwanda ya kijani ya CCM na kuandamana na vijana wasiojua mbele wala nyuma , hujigeuza kiongozi mwandamizi wa serikali na kutembelea mashule, viwanda , hospitali na ofisi za serikali. Sijui kapata wapi mamlaka haya na kwa misingi gani ya utawala bora anaweza kufanya hivi.

Viongozi wa CCM watajijengea heshima na historia kuwakumbuka, kama alivyo baba wa taifa  la Zambia, mzee Kenneth  Kaunda, kama watakubali kusoma maadishi ya ukutani na kuridhia umma unachotaka.

Kung’ang’ania madaraka, iwe kwa kutumia kauli, misuli, kupinda sheria au nguvu za dola hakusaidii. Kinachoweza kufanywa na viongozi wa CCM ni kuchelewesha mageuzi na sio kuzuia.

Upepo wa mageuzi unavuma na hauzuiliki. Kama hawataki kusoma maandishi ya ukutani hivi sasa basi watakuja kuyasoma baadaye kwa shingo upande.

Mchezo mbaya uliofanyika Dodoma wa mahesabu ya kura yasiyoeleweka na mbinu ziliotumika, ikiwa pamoja na baadhi ya wajumbe kudai vilitumika vitisho mbali ya kulazimisha kura za wazi ilikujua nani “ sio mwenzetu” sio suluhisho.

Nimeeleza mara nyingi kwamba Waswahili hawakukosea waliposema…Mambo kangaja…huenda yakaja. Sasa yanakuja. Mfano mzuri ni Zanzibar ambapo viongozi wale wale waliowaita wahaini na wasaliti hivi sasa ni sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa.

Nani alitegemea haya ukitafakari nguvu, mbinu na hadaa zilitumika kwa muda mrefu kuvunja upinzani Visiwani?

Viongozi wa CCM wanapaswa kuacha kujikaza kisabuni na huku wateketea. Ni vyema kuzima cheche za moto zilizopo ardhini kuliko kuzingojea kufika paani.

Kikundi maarufu cha dansi cha Msondo Ngoma kimetoa kibao kimoja maarufu kisemacho…Haya twende. Sasa wapinzani wameungana mikono na wanasema …Haya twende na wanakuja.

Ole wao wanaokataa kusoma maandishi ya ukutani. Kama hawatayasoma leo watasomeshwa kesho. Kila la kheri CCM na tutaikumbuka kwa mengi, yanayofaa kuzungumzwa na yake tunayoyabania moyoni mpaka wakati utaporuhusu.

Chanzo: Tanzania Daima

Advertisements

One Reply to “Wapinzani waseme ‘haya twende’”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s