Kero nyingi za Muungano zimeshapatiwa ufumbuzi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed akizungumzia suala la Muungano na kutatuliwa kwake
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed akizungumzia suala la Muungano na kutatuliwa kwake

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kamati maalumu ya wanasheria wakuu wa Serikali imeundwa kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi wa mwisho suala la mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano wajumbe wa baraza la wawakilishi wameelezwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohammed ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujuwa lini kero za Muungano zitapatiwa ufumbuzi wake ikiwemo suala la mafuta na gesi na hadi sasa kero ngapi za Muungano zimeshapatiwa ufumbuzi kwa upande wa pande mbili hizo zilizoungana.

Alisema suala la mafuta na gesi ambalo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia azimio la Baraza la wawaklishi wanataka  kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano lipo katika hatua ya ngazi ya vikao vya wanasheria wakuu wa Serikali.

“Suala hili sasa wameachiwa Wanasheria wakuu wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano Tanzania na wa Zanzibar kwa ajili ya kulifanyia kazi katika ngazi za kisheria zaidi na kitaalamu….wananchi natakiwa wawe watulivu” ‘alisema Aboud.
Alisema suala la mafuta na gesi awali ni mambo ambayo yamo katika orodha ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aboud alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zina nia thabiti za kuondosha kero zote za Muungano ili kuimarisha muungano huo na kuhakikisha haki na kila upande wa muungano inapatikana bila ya upendelezo wowote na wananchi wanafanya shughuli zao bila ya matatizo.

Waziri huyo huyo alisema katika kuhakikisha hilo linafanikiwa Rais Kikwete ameunda kamati ya pamoja inayoongozwa na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamo wa Pili wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambayo inawajumuisha wajumbe kutoka pande mbili za Muungano.

“Tokea kuanzishwa kwa utaratibu wa kuzipatia ufumbuzi kero za Muungano jumla ya changamoto 13 zimewasilishwa. Kati ya hizo changamoto sita zimeshapatiwa ufumbuzi na changamoto mbili zimo katika hatua za kukamilika na changamoto tano zimo katika kujadiliwa” alisema Aboud mbele ya wajumbe wa baraza hilo.

Akifafanua zaidi Aboud alisema katika mwaka 2012 jumla ya vikao 18 vya kutatua changamoto za Muungano vimefanyika kati ya hivyo vikao tisa vya sekretarieti, na vikao vinne vyamakatibu wakuu na vikao viwili vyangazi za mawaziri na vikao viwili ni vya kamati ya pamoja na serikali ya SMT na SMZ.

Alisema vikao vya kujadili changamoto mambo ya Muungano kuanzia ngazi za makatibu wakuu, mawaziri hadi kamati ya pamoja huwa vinagharamiwa na ofisi ya makamo wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aidha vikao vya kisekta vinavyofanyika, sekta husika inagharamia wataaalamu wake kwa vikao hivyo. Ambapo ofisi ya makamo wa pili wa rais wa Zanzibar huwa ina ratibu vikao hivyo.

Alisema tangu kuundwa kwa kamati ya kuzipatia kero za Muungano katika mwaka 2006 jumla ya kero 13 zimejadiliwa ambapo kero sita zimepatiwa ufumbuzi wake ikiwemo kuwepo kwa Tume ya haki za binaadamu na utawala bora, kuwepo kwa mfuko wa jimbo pamoja na Zanzibar sasa kukopa katika taasisi za fedha za kimataifa.

Alizitaja kero ambazo bado zinafanyiwa kazi ikiwemo mgawanyo wa mapato yanayotokana na Benki kuu, ushiriki wa Zanzibar katika jumuiya ya Afrika ya mashariki na faida zake na mfuko wa pamoja na Fedha.

Alisema katika suala la mfuko wa pamoja wa fedha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imetowa mapendekezo yake katika mgawanyo wa Fedha na kwa sasa inasubiriwa  Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia kikao cha baraza la mawaziri.

Akitaja changamoto zilizopo katika suala hilo alisema changamoto hizo zimekuwa zikitatuliwa kwa kujadiliwa na wahusika wa pande zote mbili katika ngazi za wataalamu, makatibu wakuu, mawaziri na kufikia mkutano wa kamati ya pamoja.

Akijibu suali la kiasi gani cha fedha kilichotumika katika kutatua kero za muungano, Aboud amesema hana jibu la kuwapatiwa wajumbe wa baraza la wawakilishi la kujua kiasi gani cha fedha zilizotumika tokea kuanza kwa vikao hivyo.

MWISHO

mbio za mwenge haziendeshwi kisiasa

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema mbio za Mwenge wa uhuru zimeondoshwa katika utaratibu wa kuendeshwa kisiasa na sasa zinaratibiwa na serikalini kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo nchini.

Waziri wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Zainab Omar Mohammed aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi (CUF) Saleh Nassor Juma aliyetaka kujuwa utaratibu wa kuendesha mbio za mwenge wa uhuru na kuaidia miradi mbali mbali kati ya pande mbili za Muungano.

Zainab alisema mabadiliko makubwa ya kuendesha mbio za mwenge yamebadilika kutoka katika vyama vya siasa na sasa kwenda serikalini na wananchi wamefaidika sana na mbio hizo na kuachana na tofauti zao za kisiasa hivi sasa.

Alisema utaratibu wa kuwapata wakimbi wa mwenge wa uhuru kitaifa ikiwemo kiongozi wa mbio hizo, wizara yake kwa huwa inawatangazia vijana wote raia wa Tanzania wenye sifa zinazohitajika kama vile afya njema, walimaliza kidatu cha 4, na kuendelea walio na umri wa miaka 18 hadi 35 kuomba nafasi hizo, ambapo baada ya kupokea maombi vijana hao hufanyiwa usaili na kamati maalumu iliyoteuliwa na wizara yenye uzoefu wa kuikimbiza mwenge kitaifa.

‘Tumebadilisha utaratibu wa kuendesha mbio za mwenge kutoka katika mfumo wa kisiasa na sasa kwenda katika serikali kuu ukiratibiwa na serikali mbili za jamhuri ya muungano na serikali ya mapinduzi ya zanzibar’alisema.

Alisema kwa muda mrefu mbio za mwenge zimekuwa zikiendeshwa na vijana kutoka sehemu mbili za jamhuri ya muungano wa Tanzania ambapo utaratibu wa sasa ni kupokezana kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

“Mbio za mwenge za mwaka huu kiongozi wake anatoka Zanzibar…..lakini kwa mujibu wa mabadiliko ya mbio hizo hazina makundi ya wanasiasa kutoka katika vyama” alisema Zainab.

Akijibu utaratibu unaotumika wa kuzindua mbio za mwenge na kilele chake ni mikoa yenyewe inayoomba kwa uongozi wa wizara, baada ya wizara kuridhika na sababu za maombi yao mkoa ndio wenye kupewa fursa ya kuandaa uzinduzi au sherehe za kilele hicho cha sherehe za mwenge.

MWISHO
Serikali yaahidi kuondosha tatizo la maji

Wizara ya Ardhi, Maakazi, Maji na Nishati imesema ina mpango wa kuwaondoshea shida ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa kuchimba visima tisa vya maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Waziri wa wa wizara hiyo, Ramadhani Abdallah Shaaban alisema yao wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake, Mwanaidi Kassim Mussa aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la maji katika mkoa wa mjini Magharibi na hatua zilizofikiwa katika hadi sasa.

Waziri Shaaban alisema mradi wa maji Maji wa Mkoa wa  Mjini Magharibi umekamilika tangu mwaka 2009 lakini kutokana na kutokea baadhi ya mambo fulani bahati mbaya mradi huo haukuwa na mafanikio makubwa kwa baadhi ya maeneo.

Alisema wizara yake kupitia wizara ya maji imeamua kuchimba visima tisa ili kuongeza wingi wa maji katika mkoa wa mjini magharibi na hadi sasa tayari wizara imeshachimba visima vitano, katika maeneo ya Chumbani visima vitatu na Saaateni visima viwili.

Waziri huyo alisema jitihada za kuchimba visima yengine vinne zitakamilika mara hali ya fedha itakaporuhusu.

Akijibu suali la Mwakilishi huyo aliyetaka kujua ni kiasi gani kimetumika cha fedha kwa ajili ya mradi huo wa maji, Waziri Shaaban alisema mradi wa mkoa wa Mjini Magharibi uliofandhiliwa na serikali ya Japan hadi kukamilika kwake umegharimu jumla ya shilingi za kitanzania billioni thelathini na mbili na millioni 500 (32, 500,000.00),

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichangia jumla ya shilingi ya kitanzania millioni mia mia tano (500,000.000,000). wakati serikali ya Japan ilichangia shilingi za kitanzania katika mradi huo wa maji Billioni thelathini na mbili (32,000,000,000)

Akijibu suali la asilimia ngapi kwa la wananchi wanaopata maji safi na salama katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Waziri huyo alisema, wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi wanapata maji kwa safi na salama kwa asilimia 81 kiwango ambacho ni kizuri na cha kuridhisha.

Aidha alisema wizara yake bado haijaridhishwa na na kiwango hicho na ndipo wizaraimeamua kuchimba visiwa vyengine zaidi ili kupunguza mgao wa maji ambao umekuwa ukiwasumbua wananchi wengi wa manispaa ya Zanzibar.

“Lengo la serikali ni kuondosha tatizo kabisa la maji kwa wananchi wetu hapa Zanzibar na serikali ipo katika juhudi za kutafuta njia za kuwasaidia wananchi katika tatizo hilo” aliongeza waziri huyo.

Akijibu suali la ngonyeza la Mwakilishi wa Kwahani (CCM) Ali Mussa Hassan alityetaka kujua Mkoa upi wa mji wa Zanzibar unajitosheleza kwa maji katika mikoa yote mitano ya Zanzibar, waziri huyo alisema hakuna hata mkoa mmoja katika mji wa Zanzibar ulijitosheleza kwa maji safi na salama.

MWSHO

Wizara ya biashara yatengeza billioni 300

Jumla ya Shilingi Milioni 300 za Tanzania zimetengwa na Wizara ya Biashara viwanda na Masoko katika mwaka fedha wa 2013/2014 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya ununuzi wa zao la karafuu.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Thuwaiba Edington Kisasi  wakati akijibu suala la Jimbo la Mtambwe (CUF) Salim Abdalla Hamad aliyetaka kujua kiasi gani cha fedha kimetengwa kwa ajili ya suala la zao la karafuu.

Mwakilishi huyo alitaka kujua pia ahadi iliyowekwa na wizara hiyo ya kujenga Vitua vya uuzaji wa karafuu katika kisiwa cha Pemba.

“Mheshimiwa Spika serikali kupitia wizara yake imejiwekea utaratibu wa kuvikarabati vituo vya zamani na kujenga vipya katika maeneo vipya katika maeneo ambayo serikali itaona inaona inafaa kufanya hivyo kwa azma ya kuwaondoshea usumbufu wakulima wa zao la karafuu la kutembelea masafa marefu ili kwenda kuuza karafuu zao” alisema Kisasi.

Aidha serikali kwa makusudi imeamua pia kuvifanya vituo hivyo kuwa ni kivutio kwa wakulima kwa kujenga vyoo na maeneo ya kukaa wakati wa kusubiri wauzaji wa karafuu zao pamoja na kuwapatia huduma za maji ya kunywa wakulima hao.

Akijibu suali la azma ya ujenzi wa vituo hivyo katika sehemu ya Chanjaani na Bwagamoyo imefikia wapi Naibu huyo alisema katika kutekeleza dhamira ya nzuri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kupitia shirika lake la ZSTC tayari imeshaandaa bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano mwaka huu wa fedha wa 2013/2014.

Kisasi alisema Alisema vituo hivyo vitajengwa eneo la Chanjani, Bwagamoyo,na vituo vingine vya Gando,Chambani na Wambaa.

Kisasi alisema mpango huo utaanza iwapo fedha za bajeti za wizara hiyo zitakapotengwa kama na wizara inatarajiwa kuingizwa katika mpango wa shirika la ZSTC kwa mwaka wa fedha ujao ambapo kiasi cha shilingi milioni 300 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo.

MWISHO

Kesi za ubakaji kuendeshwa haraka

Waziri wa Katiba na Sheria  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Abubakar Khamis Bakari amesema mahakama zimeanza kufanya marekebisho makubwa katika kuhakikisha kesi za ubakaji zinaendeshwa na kutolewa maamuzi haraka kwa wakati ili kuepusha malalamiko kwa jamii.

Bakary alisema hayo wakati alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura (CCM) Hamza Hassan Juma aliyetaka kujuwa kwa nini kesi za ubakaji zinachelewa kutolewa hukumu kiasi ya wahusika ikiwemo wazazi kukata tamaa.

Akifafanua Bakary alikiri yapo malalamiko mengi kutoka kwa jamii kuhusu kuchelewa kusikilizwa kesi za ubakaji pamoja na kutolewa maamuzi kutoka kwa Mahakimu na Majaji.

‘Tayari tumetowa maelekezo kwa Mahakimu na Majaji kuhusu utaratibu mpya wa kuzikilizwa kwa kesi za ubakaji katika Mahakama za Unguja na Pemba…..tunataka kesi zisikilizwe haraka kwa wakati’alisema.

Aliutaja utaratibu huo ikiwemo kubadilisha utaratibu wa ushahidi,ambapo imebainika kesi hizo kukosa watu wa kutoa ushahidi wa tukio,na matokeo yake kesi kufutwa.

‘Ushahidi katika kesi za ubakaji ni tatizo kubwa na ndiyo chanzo cha kupelekea kuchelewa kusikilizwa pamoja na kutolewa maamuzi na wakati mwengine kesi kufutwa…..wananchi wengi hawapo tayari kutoa ushahidi kwa matukio wanayoyajuwa’alisema.

Bakary ambaye alipata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema jamii haipo tayari kutoa ushahidi wa matukio mbali mbali katika mahakama.

Alisema kesi za ubakaji zinahitaji ushahidi wa kina usio shaka,ambao ndiyo utakaoweza kuwatia hatiani watuhumiwa.

Alisema huu si wakati tena wa kulinda katika matukio ya kesi za jinai ikiwemo ubakaji ambazo madhara yake kwa jamii ni makubwa.

Mapema Abubakari alikiri kuwepo kwa matukio ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja,ingawa havipo kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo alisema zipo sheria zinazodhibiti na kupambana na vitendo hivyo ikiwemo hukumu kali kuanzia miaka 30 hadi kifungo cha  maisha.

‘Sheria zetu zipo wazi katika kudhibiti na kupambana na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja……makosa ya ubakaji,ndoa za jinsia moja na umalaya hukumu zake zipo’alisema Abubakar.

Mwisho.

Advertisements

One Reply to “Kero nyingi za Muungano zimeshapatiwa ufumbuzi”

  1. kuhusu suala la muungano hizo kero nani atataua maana ukiaangalia kwa umakini na kutafakari hiki ni kiini macho 2 makamu wa rais mungano ni kutoka znz,makamu wa 2 wa smz nii mzanzibar waziri wa masauala ya muungano ni mzanzibari sasa mhe Aboud utatuambia nini sie wazanzibari kuhusu hizi kero mmepewa sumu mle wenyewe

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s